MFUKO wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) umeendelea na kampeni yake ya kutoa elimu kwa umma kuhusu utekelezaji wa miradi ya mawasiliano vijijini, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali kufikisha huduma za mawasiliano kwa wananchi wote, hususan maeneo ya vijijini.
Kampeni hii inalenga kuwafahamisha wananchi kuhusu uwekezaji unaoendelea kufanywa na Serikali kupitia UCSAF, pamoja na kuhimiza ushiriki wao katika ulinzi wa miundombinu ya mawasiliano na matumizi sahihi ya huduma hizo.
Katika kijiji cha Ibofwe, kata ya Irole, wilayani Kilolo, Serikali kupitia UCSAF imetoa ruzuku ya Shilingi Milioni 122.6 kwa kampuni ya Vodacom Tanzania kwa ajili ya ujenzi wa mnara wa mawasiliano, ambao unalenga kuondoa changamoto ya ukosefu wa mawasiliano katika eneo hilo.
Kupitia kampeni hiyo, UCSAF inalenga kuimarisha ushirikishwaji wa wananchi katika miradi ya maendeleo, kukuza uelewa kuhusu umuhimu wa miundombinu ya mawasiliano, na kuhakikisha kila Mtanzania ananufaika na mapinduzi ya teknolojia.