MAMLAKA ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) imeendelea kutumia fursa ya maadhimisho ya wiki ya utumishi wa umma yanayoendelea Jijini Dodoma katika Viwanja vya Chinangali park, kuhamasisha utalii wa ndani kwa wananchi na wadau mbalimbali waliofika kwenye banda la NCAA ndani ya Banda la Wizara ya Mali Asili na Utalii.
Wananchi waliofika kwenye banda hilo, wamesikika wakisifia huduma inayotolewa na wataalam wa Mamlaka hiyo hususani, vivutio vilivyopo ndani ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro huku wengi wao wakionekana kufurahia kupata uwelewa kuhusiana na vivutio hivyo na wengine wamekiri kuwa walikuwa hawajui historia na upekee wa eneo hilo lilosheheni vivutio vilivyobeba historia ya pekee duniani.
“Nimejisikia fahari kujua Tanzania tumebeba Historia adhimu Duniani ya Chimbuko la Mwanadamu, huu ni urithi mkubwa sana, natamani mimi na familia yangu tufike Laitole nikajione masalia hayo ya nyayo,” alisema Theresia Steven mmoja wa wakazi wa Dodoma aliyetembelea banda la NCAA.
Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yaliyoanza Juni 16, 2025 yanatarajiwa kufikia kilele chake leo, Juni 23, 2025, ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa Majaliwa.