Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
KATIKA moja ya mahojiano na kituo kimojawapo cha televisheni katika Bunge 12, Mkutano wa 19 unaomalizika Jijini Dodoma, Mbunge wa Jimbo la Konde, Kaskazini Pemba (ACT Wazalendo) anakiri kuwepo maendeleo ya miundombinu Zanzibar.
Akiwa katika mahojiano kabla ya mkutano, anasema, awali mara kadhaa alitumia fedha za mfuko wa Jimbo kuziba mashimo au wakati mwingine kukwangua kwa greda ili ziweze kupitika.
Anabainisha kuwa, kutoka jimboni kwake hadi Micheweni ambako ndipo ilipokuwa Hospitali ya wilaya, ilikuwa changamoto kubwa; kutokana na ubovu wa barabara.
“Jamii iliona bora mjamzito kujifungulia nyumbani kuliko kwenda hospitali wilayani kutokana na mashimo katika barabara, lakini hali sasa ni tofauti” anasema.

Anasema, barabara za lami zimejengwa zikiwemo za ndani na kikubwa huduma zote za kijamii walizokuwa wanazifuata wilayani zipo jimboni.
Si mbunge huyo pekee yake ambaye barabara za jimbo lake zilikuwa hazipitiki, bali pia majimbo mengine na wakati wote, Serikali ilitenga pesa, zikakwanguliwa, kuzibwa mashimo.
Katibu Kamati Maalum NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo Khamis Mbeto Khamis anasema kila mwaka pesa ilitengwa kwa ajili ya matengenezo madogo madogo ikiwa ni pamoja na kuziba mashimo kwa kuweka viraka na kifusi.
Mwenezi Mbeto anasema, baada ya mwaka mmoja au miwili, zinaharibika tena na kukabili hali hiyo, Dkt. Mwinyi akaja na ubunifu ambao unafanya Zanzibar hivi sasa kuwa na barabara zenye hadhi ya Kimataifa.
“Rais ametumia akili kubwa kwa kutaka pesa zilizokuwa zinatengwa kwenye bajeti ya Serikali kwa ajili ya kuziba mashimo barabarani kila mwaka zikusanywe” anasema Mbeto.

Fedha zingine ni zile zinazotokana na Shilingi 100 inayokatwa na kusanywa kwa ajili ya kuhudumia barabara na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (ZURA), katika kila lita ya mafuta inayouzwa.
“Zanzibar kila mwezi tunatumia lita Milioni 15 za mafuta kuanzia ya magari hadi ya ndege, piga hesabu ya TSh. 100 kwa kila lita” anasema.
Pia, anabainisha, tozo za kisheria za leseni za barabara (Road Licence) ambazo zinaenda mfuko wa barabara na ndio maana serikali ikaamua bora kukopa na kujenga barabara zote, ikusanye ilipe.
Anasema, hakuna anayebebeshwa mzigo wa deni hilo kama baadhi ya wanasiasa wa upinzani visiwani humo wanavyodai na ana wasiwasi juu ya uwezo wao wa kufikiri.
“Fedha tulizonazo ni nyingi kuliko mkopo unaotolewa na ndio maana serikali inamudu kulipa” anasema.

Anasema, Ilani ya CCM ilimpa Rais Dkt. Mwinyi atekeleze ujenzi wa Kilometa 96 za barabara lakini yeye kajenga Kilometa 1000 ikiwa ni wastani wa asilimia 1000.
Mbeto anasema, leo muonekano wa Mpendae, Magogoni, Mbweni ambako barabara zote ni za lami ni tofauti sana na hapo awali na imeongeza thamani ya maeneo hayo.
Mbeto anasema, barabara ya Kinazini-Bububu ambayo ilijengwa na Kampuni ya Kajima enzi za Hayati Rais Aboud Jumbe hivi sasa njia nne.
Madaraja yanajengwa na msongamano unapungua na barabara mpya ya Mwanakwerekwe/Amaan imeondoka.
Anasema daraja lenye urefu wa Kilometa 3.5 linajengwa Kusini/Uzi likiwa njia nne jambo ambalo halikuwahi kufikiriwa.

Ilani ijayo 2025/2030 ya CCM, anasema Mbeto inataja ujenzi wa daraja kuunganisha Mkokotoni na Tumbatu.
“Hiyo ndio maana ya miundombinu na uchumi na sasa tunakusanya fedha, tunalipa deni na zingine zinabaki kwa ajili ya matengenezo na usimamizi wa hizo barabara,” anasema Mbeto.
Mwenezi huyo anasema, hivi sasa Serikali inajenga barabara ya Tunguu, Makunduchi hadi Kizimkazi zikiwa na taa mwanzo, mwisho.
Pia, barabara ya Kilometa 13 Kisauni hadi Fumba achilia mbali barabara za mjini za kutoka Hospitali ya Mnazi Mmoja hadi Malindi na ile ya Michenzani.
“Leo tunatekeleza sera ya uwekezaji, wakija kitu cha kwanza wanauliza miundombinu” kama huna barabara unamvutiaje.
Mbeto anasema ukijenga miundombinu, unajenga uchumi imara kwani ni rahisi kumvutia mwekezaji.
Uchumi wa Zanzibar unakua kwa asilimia saba ikiwa kinara juu ya nchi zingine za Afrika na moja ni uwekezaji na utalii na hayo ndio anayofanya Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi.