NAIBU Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Khamis Hamza Khamis ametoa wito kwa wadau katika sekta ya utalii kuongeza uwekezaji na juhudi za pamoja katika usimamizi wa utalii katika maeneo yanayolindwa ili kuwa na Utalii endelevu.
Khamis ameongeza kuwa, kuwekeza katika utalii wa maeneo yaliyolindwa sio tu kunafaida kwa uhifadhi, bali pia unahamasisha maendeleo ya kimkakati ya jamii inayozunguka maeneo hayo.
Akifungua warsha ya kujadili umuhimu wa Uhifadhi, Ukuaji wa Utalii na Ustawi wa Jamii iliyofanyika kwenye hotel ya Mt. Meru jijini Arusha alisema, ni wakati sasa wadau kujitokeza kwa wingi kuwekeza na kujikita katika usimamizi wa Rasilimali za utalii ili ziweze kutuletea faida kwa jamii na Taifa kwa ujumla.
Pia, amesisitiza juu ya umuhimu wa kubadilishana uzoefu utakaosaidia katika kuchunguza fursa zilizopo kwenye Maliasili zitakazoweza kunufaisha jamii kama kichocheo muhimu cha maendeleo.
Alisema, bila wanyama hakuna Utalii, bila misitu hakuna utalii, hivyo ni vyema tukahamasisha watu kutumia nishati safi ili kuendelea kutunza misitu yetu, kulinda na kuhifadhi wanyama wetu ili utalii uendelee na uingize pato kwa Taifa na jamii ya maeneo husika ipate manufaa.