Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
CHAMA cha Mapinduzi (CCM), kimesisitiza kuchukuliwa hatua kali za kisheria kwa mtu au kikundi cha watu ambacho kitapandikiza siasa za ubaguzi wa aina yoyote uwe wa dini au ukabila.
Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis, ameeleza hayo Juni 14, 2025, Zanzibar kuwa Sheria ya Usajili wa Vyama Vya Siasa Namba 5 ya Mwaka 1992, inakataza matumizi ya siasa za ubaguzi wa aina yoyote, udini na ukabila.
Kutokana na kuwepo kwa sheria hiyo, Mwenezi Mbeto ametaka mikono ya sheria iwashughulikie wale wote wanaovunja sheria hiyo wakiwa na wengine wakiwa wameanza kupanda mbegu hiyo katika jamii.
Mbeto alisema, sheria ni msumeno hivyo mtu au watu wanaofikiri wanaweza kufanikisha mradi huo wa hatari wa kuwagawa wananchi, washughulikiwe mapema, kwani kuruhusu hali hiyo ni kuhatarisha usalama wa nchi na watu wake.
Alisema, kuna mifano ya nchi nyingi ambazo zimekumbwa na madhira makubwa na maafa kutokana na watu wachache kuachwa wakihubiri uchochezi wa ubaguzi wa kikabila na dini, hivyo mambo hayo yasiachwe yachipue, yakue na kustawi.
“Kuna baadhi ya wanasiasa kutokana na kufilisika kwao kisiasa, wameanza kutumia lugha za ubaguzi, udini na ukabila wadhibitiwe na sheria zipo hivyo ni vema zikafuata mkondo,” alisema Mbeto.
Katibu huyo Mwenezi alisema, nchi ina maadui watatu ambao ni ujinga, umasikini na maradhi, lakini pia maadui wa usalama wa Taifa na amani yetu ni ubaguzi wa udini na ukabila.
“Vyama vyote vya Siasa vina sera zake. Program za kisiasa na kioganaizesheni. Ikiwa vipo vyama havina sera viache siasa. Kutumia ukabila, udini na ubaguzi katika siasa ni kwenda kinyume na sheria,” alieleza.
Alisema, hivi sasa kuna baadhi ya vyama vya siasa, uongozi wote wa juu umeshikwa aidha na viongozi wa dini moja na mbaya zaidi unaweza ukakuta wanatoka kanda moja, pia si ajabu wakawa kabila moja, jambo ambalo ni hatari kwa ustawi wa Taifa.
Mbeto alibainisha kuwa, endapo sheria zinazopiga marufuku mambo hayo hatari kwa Taifa zitakaa kimya, kadri siku zinavyokwenda mbele, itaonekana masuala hayo ni mambo ya kawaida, hivyo Taifa litagawanyika na kuingia katika sintofahamu.