BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imeendesha mafunzo ya uwekezaji katika dhamana za Serikali kwa watumishi wa Halmashauri na viongozi mbalimbali.
Akizungumza katika semina hiyo, mkufunzi David Mponela alisema, Serikali imeamua kutoa elimu hiyo kutokana na uelewa mdogo wa wananchi kuhusu fursa za uwekezaji, hali inayowafanya kukosa njia za kujiongezea kipato na kusaidia maendeleo ya taifa.
“Watanzania wakielimika kuhusu uwekezaji, wataweza kusaidia serikali kupata fedha kwa ajili ya miradi mikubwa ya kimkakati, huku nao wakijiinua kiuchumi,” alisema Mponela.
Naye mkufunzi Johnfas Gwagilo aliwahimiza watumishi kuanza kuwekeza mapema wakati bado wako kazini ili kujitayarisha na maisha ya baada ya kustaafu.
Watumishi wa Halmashauri hiyo wameishukuru serikali kwa kuwafikishia elimu hiyo muhimu, wakisema itawasaidia kufanya maamuzi bora ya kifedha na kuongeza ustawi wao binafsi.