CCM waitaka ACT kuacha kuchochea vurugu Z’bar

0

Na Mwandishi Maalum, Zanzibar

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM ) kimekitaka ACT Wazalendo kuacha kueneza upotoshaji na kudai kuwa uandikishaji wapiga kura Mikoa wa Kaskazini ” A” na ‘B’ kuna baadhi ya wananchi hawakuandikishwa.

CCM kimekanusha na kusema, wananchi wote waliokidhi vigezo kwa vya sheria ya Ukaazi na majina yao yamo kwenye Daftari la Sheha wa shehia, wote wameandikishwa.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Mbeto Khamis Mbeto, ambapo amemtaka Naibu Katibu Mkuu ACT Wazalendo Zanzibar, Omar Ali Shehe na kumtaka aache kutengeneza madai ambayo hayana ukweli.

Alisema, Shehe amekuwa akitoa madai ya uongo dhidi ya watendaji wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC ), Kamati za Ulinzi na Usalama Mikoa, Wilaya na Makatibu Tawala SMZ kila wanapotimiza majukumu yao ya kazi.

“Shehe kila wakati amekuwa kiongozi kichefuchefu anayekusudia kuvuruga taaswira ya utulivu katika uandikishaji wapiga kura. SMZ ina Vyombo vyake vya Kiserikali kuanzia Shehia hadi Serikali Kuu,” alisema Mbeto.

Alisema, kwa kiongozi anayejua mgawanyo wa madaraka wa Serikali, hawezi kumzuia Mkuu wa Mkoa, Wilaya, Polisi, Maafisa wa Usalama au Makatibu Tawala wilaya na Mikoa, wasitimize wajibu wa kazi zao.

Mbeto alisema, Omar Shehe anaonyesha hatambui hadhi ya vyombo na pengine haujui hata muundo wa Serikali, hivyo amekuwa akilipuka na kutoa shutuma, akieneza uzushi na kufanya upotoshaji wakati zoezi la uandikishaji likiendelea vizuri.

“Kinachofanywa na Omar Shehe ni utekelezaji wa mpango mkakati wao batili kuelekea uandikishaji Wilaya na Mikoa mingine ya Unguja. Anatamani uzuke mtafaruku. Wanaochochea na walioandaliwa kufanya fujo watajulikana,” alieleza.

Mbeto katika maelezo yake alisema, ACT wanajiandaa kuvunja sheria kwa kujaribu kutaka kuwazuia watanzania waliotimiza vigezo vya kisheria baada ya kukaa Zanzibar miaka kumi mfululizo jambo ambalo si sahihi kwa mujibu wa sheria.

“Sheria Namba 4 ya Mwaka 2018 imetaja mzanzibari aliyeishi kwenye jimbo na shehia miezi thelathini na sita mfululizo ataandikishwa kuwa mpiga kura. Kwa Mtanzania anayetoka aidha Mara, Njombe, Sumbawanga au Mbeya aliyeishi Zanzibar miaka kumi mfululizo nae ana haki ya kuandikishwa na kupiga kura,” alieleza Mbeto.

Mwenezi huyo wa CCM alisema, mara kadhaa amekuwa akimsihi Shehe aepuke kutoa matamshi hatarishi badala yake aonyeshe ukomavu wake kisiasa, lakini amekuwa akijifanya haambiliki na hamnazo.

“Zoezi la uandikishaji linaendelea vizuri. CCM imeshakusanya ushahidi wa matamshi ya vitisho yaliyotamkwa na viongozi wa ACT kwenye mikutano ya hadhara. Tumevijulisha vyombo vya dola vipime matamshi hayo na kuchukua hatua mapema,” alieleza Mbeto.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here