TCB yazindua huduma ya ‘Kikoba Kidigitali’

0

Na Mwandishi Wetu

BENKI ya Biashara Tanzania (TCB), imeanzisha huduma ya Kikoba Kidigitali itakayokuwa rahisi kwa watumiaji wa Kikoba kuweka fedha na kukopeshana.

Kwa miaka ya karibuni kumekuwa na vikundi kadhaa vya vikoba kupitia mitandao ya simu na humo wanachama huweka akiba na kukopeshana kwa riba nafuu na TCB ndio inayohusika na huduma hiyo ya fedha kwa kushirikiana na mitandao ya simu.

Vikoba hivyo huvunjwa baada ya mwaka mmoja na vingine huvunjwa baada ya miaka mitatu hadi mitando na wanachama kugawana faida kabla ya kuanza kuwekeza tena.

Akizungumza katika uzinduzi wa huduma hiyo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa TCB Adam Mihayo alisema, mapinduzi waliyofanya yataboresha dhana ileile inayotumika katika vikundi vilivyozoeleka vya kuweka akiba na kukopeshana.

Mapinduzi hayo ni kuwa na kikoba chenye wanachama wanaotumia mtandao mmoja wa simu na kingine kikoba mix kitakachohusisha wanachama wa mitandao tofauti.

Katika kikao kazi kinachoandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina kati ya Wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari na taasisi za serikali, ilijitokeza hoja ya kuwa mwanachama wa kikoba kwa mitandao tofauti ya simu, jambo ambalo Mihayo aliahidi kulifanyia kazi haraka na jana amezindua kikoba kidigitali kilichokuja na suluhisho hilo.

“Tunawasogezea wateja wetu huduma hii viganjani mwao ikiwa na ufanisi zaidi na urahisi maradufu…ubunifu huu ni hatua muhimu katika sekta ya kibenki katika ulimwengu huu wa kidigitali,” alisema.

Alisema, huduma hiyo inapatikana kwa urahisi zaidi kupitia simu za mkononi na benki hiyo imeshirikiana na kampuni zote za simu nchini ikiwemo Airtel, Tigo, Vodacom na Halotel ili kurahisisha namna ya kujisajili na kujiunga na kikoba mtandaoni.

“Ukiwa na kikoba mtandaoni ni salama zaidi ni rahisi kuona miamala yako na inaleta uwazi kati ya kikundi chenu cha kikoba,” alisema.

Akifafanua zaidi Mihayo alisema, Kikoba Kidigitali kitakuwa na aina mbili ya vikoba, ya kwanza ni ile ya mteja kujisajili au kujiunga na kikoba kupitia mtandao wake wa simu, hicho inaweza kuwa kwa ajili ya Marafiki na familia walio kwenye mtandao mmoja.

“Aina ya pili ni kikoba mix ambacho hicho kinawezesha watu kutoka mitandao tofauti kuunganika kwa pamoja na kuunda kikoba kwa namba zao na ili ufungue kikoba mix utapiga 15021# na utapelekwa moja kwa moja kwenye menu ya TCB utafuata maelekezo rahisi,” alisema.

Mihayo alisema Kikoba ni zaidi ya fursa ya kidigitali kwani inabeba dhana pana ya uwazi, ujumuishi na usalama katika uwekaji wa akiba na usimamizi bora wa kifedha tukitumia nyenzo hii ya teknolojia tunaviwezesha vikundi nchini kote kusimamia mategemeo yao ya kiuchumi, kukua kiuchumi na kujitegemea,” alisema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here