ZFDA yapiga marufuku bidhaa za virutubisho

0

WAKALA wa Chakula na Dawa Zanzibar (ZFDA) imepiga marufuku uingizaji wa bidhaa za virutubisho vyenye mchanganyiko wa dawa za hospitali kutokana na madhara ya kiafya yanayoweza kujitokeza kwa watumiaji, hasa wale wanaovitumia bila ushauri wa kitaalamu kutoka kwa madaktari.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Mkurugenzi Mtendaji wa ZFDA, Dkt. Burhani Othman Simai, alisema virutubisho hivyo vimekuwa vikiingizwa nchini kinyume cha sheria na kubainika kusababisha madhara kwa afya ya binadamu.

Alifafanua kuwa, katika kipindi cha miezi miwili, ZFDA kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi ilikamata shehena ya takriban tani 2.5 za virutubisho hivyo vilivyoingizwa kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Zanzibar.

“Watumiaji wengi hawazingatii ushauri wa kitaalamu na hawajui madhara makubwa wanayoweza kuyapata, hasa wanapotumia virutubisho hivi bila usimamizi wa daktari,” alisema Dkt. Burhani.

Virutubisho hivyo vinadaiwa kuongeza hamu ya tendo la ndoa na kukuza maumbile ya sehemu za siri, na mara nyingi huchanganywa na asali au chocolate ili kuwavutia watumiaji. Baadhi ya bidhaa zilizotajwa ni pamoja na Royal Honey, M Plus, Etuma na Gold Q7 Chocolate.

Kwa mujibu wa ZFDA, madhara yanayoweza kujitokeza ni pamoja na kifafa, mshtuko wa moyo, kifo cha ghafla (hasa kwa wagonjwa wa VVU wanaotumia dawa za ARV), kupungua kwa uoni na usikivu, pamoja na kushindwa kushiriki tendo la ndoa mara baada ya kuacha matumizi ya virutubisho hivyo.

Kutokana na hatari hizo, ZFDA imesisitiza kuwa itaendelea kuchukua hatua kali kwa yeyote atakayekiuka agizo hilo, na kuwataka wananchi kutoa taarifa mara wanapobaini uwepo wa bidhaa hizo katika maeneo yasiyo rasmi.

Aidha, Dkt. Burhani alibainisha kuwa ZFDA itaendeleza ushirikiano na vyombo vya usalama ili kudhibiti uingizaji wa bidhaa zisizosajiliwa na kuwaelimisha wananchi kuhusu matumizi salama ya chakula, dawa, vipodozi na vifaa tiba.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here