Zanzibar sasa yakopesheka, fedha za akaunti maalum zafikia dola Milioni 350

0

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema kuwa fedha zilizopo katika Akaunti Maalum ya Kulipia Madeni zimefikia Dola za Kimarekani Milioni 350, hatua ambayo imeiwezesha Zanzibar kukopesheka na kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo kwa kutumia fedha za ndani.

Akizungumza leo Oktoba 27, 2025 katika hafla ya utiaji saini wa mikataba ya miradi mitatu mikubwa ya kimkakati iliyofanyika Ikulu Zanzibar, Dkt. Mwinyi alisema hatua hiyo ni mafanikio makubwa yanayoimarisha uchumi wa Zanzibar na kuonesha nidhamu bora ya kifedha ya Serikali.

Mkataba wa Mradi wa Mfumo Jumuishi wa Usimamizi na Usajili wa Huduma za Ardhi Zanzibar (LARIS) ulitiwa saini kati ya Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Mussa Nsekela, na Makamu wa Rais wa Kitengo cha Ufadhili wa Biashara wa BPI France, Alienor Daugreilh.

Kwa upande wa Mradi wa Usambazaji Maji Mkoa wa Kusini Unguja, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliwakilishwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Nishati na Madini, Joseph John Kilangi, na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Next Health Digital Solution BV kutoka Uholanzi Subrahmanyam Yadavalli.

Aidha, Mkataba wa Ujenzi wa Kituo cha Huduma za Saratani Binguni ulitiwa saini kati ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Mngereza Mzee Miraji, na Mwenyekiti wa Bodi na Mkurugenzi wa Kituo cha Aegle Onco Care Center Limited, Dkt. Diara Pankaj Wadhwa.

Dkt. Mwinyi alieleza kuwa Serikali imeweka utaratibu wa kujiwekea akiba ya Dola Milioni 15 kila mwezi, sawa na Dola Milioni 180 kwa mwaka, hatua inayoongeza uaminifu wa Zanzibar katika taasisi za kifedha na kuongeza uwezo wa kulipa madeni kwa wakati.

Halikadhalika, Dkt.Mwinyi alisema kuwa utaratibu huu umeiwezesha Serikali kutekeleza miradi mikubwa kwa kutumia fedha za ndani kwa hatua ya kujitegemea na kujenga uchumi imara

Amesema miradi hiyo mitatu itamaliza changamoto za muda mrefu zikiwemo ukosefu wa maji Kusini Unguja, migogoro ya ardhi, na gharama kubwa za matibabu ya saratani, ambapo sasa wananchi watapata huduma hizo ndani ya Zanzibar.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here