Na Mwandishi Wetu
WAKALA wa Vipimo (WMA) umewahimiza watanzania kuchangamkia fursa za kazi za vipimo nchini Zambia kufuatia mkataba wa ushirikiano uliosainiwa Disemba 11, 2025.
Mkataba huo wa miaka mitatu, ulisainiwa jijini Lusaka, Zambia baina ya WMA na Wakala wa Vipimo Zambia (ZMA) unalenga kuweka mazingira rafiki ya ufanyaji biashara kwenye sekta ya vipimo.
Akizungumza kwenye mahojiano maalumu jijini Dar es Salaam, Afisa Mwandamizi wa WMA Renatus Mathayo alisema, wamekuwa na ushirikiano wa kawaida na ZMA na wamekuwa wakikutana kwenye majukwaa mbalimbali, lakini hivi sasa wameamua kupiga hatua kubwa zaidi.
Alisema, kama alivyosema Afisa Mtendaji Mkuu wa WMA, Alban Kihulla baada ya kusainiwa mkataba huo wa ushirikiano, Makampuni ya Tanzania yanapaswa kwenda Zambia kuomba kazi ya kufanya baadhi ya majukumu ya Wakala wa Vipimo na wamekuwa wakitoa leseni kwa sekta binafsi kwa ajili ya kutekeleza majukumu hayo.
“Kuna kazi ambazo sisi tunazifanya, lakini wenzetu bado hawajazianza, hivyo tunafungua fursa sio kwetu tu (WMA) lakini kwa watanzania, waende Zambia kufanya kazi, Wakala wa Vipimo inashirikiana na sekta binafsi, kuna watu wanapewa leseni kwa ajili ya kutekeleza majukumu ya Wakala wa Vipimo,”
“Hiyo fursa imepatikana Zambia, hata Mtendaji Mkuu aliwaambia watanzania wenye Makampuni waende Zambia kutafuta fursa kwasababu yeye kazi ameshaimaliza,” alisema Mathayo.
Mbali na fursa hiyo, Mathayo alisema mkataba huo utasaidia kupunguza usumbufu na vikwazo, ambapo Mataifa hayo mawili yatatambua matokeo ya vipimo kutoka taifa jingine, ambapo mzigo mfano roli la mafuta likishakaguliwa Tanzania, hakuna sababu ya kukaguliwa na kutiliwa wasiwasi likifika Zambia.
“Mkishasaini mikataba mikubwa ya mashirikiano hata mkienda kule wenzenu hawana mashaka, wanawaamini kwasababu mmekubaliana kuwa na ushirikiano kwenye baadhi maeneo,” alisema.