Na Mwandishi Wetu
BONANZA lililoandaliwa na Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA) ‘Vipimo Bonanza,’ limefanyika Jumamosi, Agosti 31, 2024 kwenye viwanja vya TCC Club Chang’ombe (Gwambina) jijini Dar es Salaam na kuhusisha michezo mbalimbali.
Michezo ambayo imeshindanishwa kwenye bonanza hilo ni mpira wa miguu, mpira wa pete (netiboli), drafti, karata na kuvuta kamba na kuwakutanisha watumishi wa WMA kutoka sehemu mbalimbali.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kaimu Mkurugenzi Huduma za Biashara WMA, Karim Mkorehe alisema, limeandaliwa kwa ajili ya kujiandaa na Mashindano ya Mashirika ya Umma, Makampuni na Taasisi Binafsi nchini (SHIMUTA) yanayotarajia kufanyika Mkoani Tanga, Novemba mwaka huu.
Alisema, mbali na maandalizi ya michuano hiyo, ‘Vipimo bonanza’ limelenga kuwajengea watumishi wa WMA utamaduni wa kufanya mazoezi ili kuimarisha afya zao na kupambana na magonjwa yasiyoambukiza na hivyo kuchochea utimamu wa mwili na akili ili kuboresha utendaji wao.
Aidha, Mkorehe alisema, kwenye bonanza hilo mbali na michezo iliyoandaliwa, watumishi na wadau wengine waliohudhuria, watapata huduma bila malipo ya vipimo na ushauri kwa ugonjwa wa Homa ya Ini (Hepatitis B), Virusi vya UKIMWI (VVU), presha na Kisukari.
“Naibu Waziri Mkuu aliagiza Mashirika na wakala za Serikali kuhakikisha zinashiriki katika michezo na mashindano ambayo yanaenda kuandaliwa, tupo hapa kwenye bonanza hili kwa ajili ya maandalizi ya Mashindano hayo, sambamba na kuwapa watumishi mazoezi ili waweze kutimiza vizuri majukumu yao, nawasihi watumishi waendelee na mazoezi hadi mashindano yatakapokaribia,” alisema Mkorehe.
Kwa upande wake Oscar Ng’itu ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Sheria WMA, akizungumza kwa niaba ya wachezaji wa mpira wa miguu alisema, bonanza hilo ni muhimu wakati huu wakielekea kwenye Mashindano ya SHIMUTA na wanatarajia utawekwa utaratibu wa kila wiki au mwezi kuwepo kwenye viwanja hivyo vya Gwambina kwa ajili kujiweka sawa kiafya.
“Mazoezi haya yatatusaidia kujiweka vizuri kiafya na kujiandaa kwenye michuano ya SHIMUTA, nawasihi watumishi wa taasisi nyingine washiriki kwenye michezo mbalimbali kwa ajili ya kuimarisha afya zao,ukiwa na afya bora,hata kuwajibika unawajibika vizuri,” alisema Ng’itu na kuongeza kuwa, wanaamini watafanya vizuri kwenye mashindano hayo kutokana na maandalizi wanayofanya.
Naye, Mwakilishi wa timu ya netiboli ya WMA, Hamida Salum alisema, mbali na maandalizi ya michuano ya SHIMUTA, ushiriki wao kwenye bonanza la Vipimo, utawasaidia kujiweka timamu kiakili na kimwili ili waweze kutimiza vizuri majukumu yao ya kila siku.