Wilaya ya Kusini Magharibi yasikia kilio cha wajane

0

MKUU wa Wilaya ya Magharibi ‘B’, Amour Yussuf Mmamga, amesema Ofisi yake imeandaa programu maalum kwa ajili ya kuwasikiliza wajane, inayotarajiwa kufanyika leo, Agosti 2, 2025 katika Skuli ya Mama Samia, Mwanakwerekwe.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Mmamga amesema Ofisi ya Wilaya imekuwa ikipokea malalamiko mengi kutoka kwa wajane kuhusu changamoto mbalimbali zinazowakabili, hivyo kuona haja ya kuwa na jukwaa maalum la kuwasikiliza na kuwasaidia.

“Lengo la programu hii ni kuwaunganisha wanawake hawa na taasisi mbalimbali zinazoweza kuwapa msaada wa kisheria, ushauri wa kijamii, pamoja na fursa za kiuchumi na kijamii,” alisema Mkuu huyo wa Wilaya.

Programu hiyo imepewa kaulimbiu isemayo: “Kilio chako kimesikika, furahia neema”, na inatarajiwa kuwahusisha zaidi ya wajane 300 kutoka Shehia 30 za Wilaya ya Magharibi B. Miongoni mwa huduma zitakazotolewa ni:

Ushauri wa kisheria na mirathi Huduma za afya Usajili wa huduma Elimu juu ya haki na sheria, Kuoneshwa fursa mbalimbali za kujikwamua kiuchumi

Aidha, Mmamga alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kuimarisha juhudi zake za kuwasaidia wanawake kupitia program na fursa mbalimbali zinazolenga kuinua hali zao kiuchumi na kijamii.

Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Wilaya ameeleza kuwa changamoto kama kutelekezwa, kudhalilishwa, na kunyimwa haki bado zinawakabili wanawake wengi, hivyo programu hii inalenga kusaidia kupunguza changamoto hizo kwa njia ya ushirikiano na taasisi za kijamii na kiserikali.

Sambamba na hayo, Mmamga amezindua rasmi programu hiyo na kuwataka wajane wote waliopatiwa koponi kupitia masheha wao kufika mapema katika eneo la shughuli siku ya tukio.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here