Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
SERIKALI imeendelea kuweka mazingira wezeshi yanayozidi kuvutia wawekezaji wa kigeni kuja kuwekeza hapa nchini hususani katika sekta ya usafirishaji.
Akizungumza na waandishi wa habari kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo Plasduce Mbossa, Afisa Mwandamizi wa Masoko Nocha Samweli alisema, utendaji kazi wa bandari kwa sasa umeendelea kuleta matokeo chanya na kurahisisha utoaji huduma kwa wadau mbalimbali wanaotumia bandari ya Dar es Salaam na zinginezo.
Samweli alitoa rai kwa wananchi wote kwenda kwenye banda lao kujifunza masuala mbalimbali yanayohusu usafirishaji wa shehena majini pamoja na mbinu mbalimbali za biashara na kuwataka wazichangamkie.
Kwa upande wake Meneja Uhusiano wa Shirika la Bandari Zanzibar Hassan Amour alisema wanashiriki maonesho hayo kwa mara ya pili wakiwa na lengo la kuendelea kuelimisha umma kuhusiana na utendaji kazi wa bandari ya Zanzibar na miradi ambayo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wanaitekeleza.
“Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kujenga bandari kadhaa kwa lengo la kuendelea kukuza biashara katika visiwa vyetu na kuondoa utegemezi wa bandari moja pekee,” alisema Amour.
Amour alitaja baadhi ya bandari ambazo zinajengwa na Mamkala hiyo ni pamoja na Ujenzi wa Bandari ya Fumba iliyoko katika Wilaya ya Magharibi B Unguja, Ujenzi wa bandari kavu ya Maruhubi, Ujenzi wa Bandari ya abiria ya Maruhubi Mpiga duni, na ujenzi wa bandari Jumuishi Mangapwani, pamoja na bandari nyinginezo.
Aidha, Amour alisema bandari za Zanzibar zinachangia asilimia 80 ya mapato yote ya Zanzibar, ndiyo maana wanaendelea kuboresha na kujenga bandari ili kukuza uchumi wa Zanzibar na kuweza kuwahudumia wananchi wake kwa kiasi kikubwa.
Naye, Mkuu wa Idara ya Biashara ya kampuni ya East Africa Gate Away Corporation ambao ni wawekezaji kwenye gati namba 8 hadi 11, Donald Talawa alisema maonesho ya Sabasaba yamekuwa na tija kwani ni mahali pekee kwa kukutana na wateja kutoka ndani na nje ya nchi.
“Haya ni maonesho ya Kimataifa, hivyo kupitia maonesho haya, tunakutana na wateja wa ukanda wote wa Afrika Mashariki na Kati ambao wanatumia bandari ya Dar es Salaam, hivyo kupitia maonesho haya tunatarajia kukutana na waterjet wengi kutoka kwenye ukanda huu,” alisema Talawa.
Sambamba na hayo, aliishukuru Serikali kupitia TPA kwa kuruhusu kampuni binafsi kuwekeza kwenye Mamlaka hiyo na kusema takwimu zinaonesha kuwa mafanikio yamekuwa makubwa kwa kuongezeka kwa wateja pamoja na mapato.
Kwa upande wake Msimamizi wa idara ya fedha kutoka DP World, Priscilla Mkumbi alisema kuwa wameamua kuhudhuria maonesho hayo ili waendelee kuelimisha Umma kuhusiana na utendaji kazi wao na kufungua njia kwa wafanyabiashara wenye uhitaji wa kuagiza mizigo nje ya nchi.
“Sisi ni mojawapo ya kampuni ya Kimataifa inayohusika na uendeshaji wa bandari mbalimbali za mataifa mbalimbali, hivyo tunajiamini na kazi yetu kwani historia inatubeba na tuna kila kitendea kazi cha kisaa kinachihitajika”, alisema Mkumbi.
Mkumbi pia alielezea tija inayopatikana kutokana na uwekezaji huo ni pamoja na kutoa ajira kwa Watanzania katika idara za udereva, ulinzi, na idara nyingine za uongozi.
Maonesho ya Kimataifa ya Dar es Salaam maarufu kama Sabasaba yamekuwa yakipanda thamani yake kila mwaka, kwani inawakutanisha wafanyabishara kutoka pande mbalimbali za Dunia kuja kuonesha bidhaa na kutafuta masoko sambamba na kubadilishana uzoefu.