Waziri Kikwete anena mazito wakati akikabidhi Mwenge

0

Na John Mapepele

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi Vijana Ajira na Wenye Ulemavu Ridhiwan Kikwete leo Oktoba 15, 2024 amekabidhi mwenge na Bendera ya Taifa kikosi cha wapiganaji ili kupeleka kwenye kilele cha Mlima Kilimanjaro ikiwa ni maelekezo aliyoyatoa Rais jana wakati wa tukio la kuzima mwenge kwa mwaka 2024 mkoani Mwanza.

Katika hafla hiyo ya kukabidhi iliyofanyika kwenye lango la Marangu katika Ofisi ya Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro Kikwete alisema, lengo la kupandisha mwenge ni kuionyesha dunia kuwa hata baada ya miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar bado Muungano huo umeendelea kuwa imara.

Aidha, alisema kupandisha mwenge katika kilele cha Mlima Kilimanjaro ni kuendelea kutangaza Mlima Kilimanjaro ulimwenguni na vivutio mbalimbali vya Utalii vilivyopo nchini.

Aliongeza kuwa, katika kipindi hiki ambacho dunia inapitia mabadiliko makubwa ya tabia nchi kupandishwa kwa mwenge katika kilele cha Mlima Kilimanjaro ni kuendelea kutoa wito wa kushiriki kikamilifu kwenye uhifadhi.

Akimkaribisha Waziri Kikwete ambaye ndiye alikuwa mgeni rasmi wa shughuli hiyo waziri wa Maliasili na Utalii alisema Mlima Kilimanjaro umebarikiwa kuwa na sifa nyingi mbali ya kuwa ni Mlima mrefu.

” Hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro ni moja ya urithi wetu mkubwa. Mlima huu sio tu ni mrefu zaidi barani Afrika, bali pia unawakilisha urithi wa dunia, uliotangazwa rasmi mwaka 1987 na UNESCO. Ni kivutio cha utalii cha kipekee ambacho kimeleta heshima kubwa kwa Tanzania kwa kushinda tuzo za kivutio bora barani Afrika kwa miaka kadhaa mfululizo”

” Ni fahari yetu, si kwa sababu ya urefu wake pekee, bali pia kwa mandhari yake ya asili inayovutia na kwa kuwa chanzo kikuu cha maji kwa mikoa ya Kilimanjaro na jirani.” alifafanua Chana.

Aidha amesema tukio hili linafanyika ikiwa imepita miaka 60 tangu tupate Uhuru, miaka 60 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar, na miaka 60 ya Muungano wetu wa Tanganyika na Zanzibar,ambapo tuna kila sababu ya kujivunia mafanikio tuliyoyapata. Hii ni pamoja na miaka 60 ya whifadhi zetu za Mikumi na Ruaha, ambazo zinachangia pakubwa katika sekta ya utalii nchini.

Ameongeza kuwa
Mwenge wa Uhuru ulipandishwa kwa mara ya kwanza mwaka 1961, wakati nchi yetu ilipopata Uhuru na Kapteni Alexander Nyirenda, , na hivyo kuweka alama ya kudumu ya uhuru wetu. Tangu wakati huo, kila tunapopandisha Mwenge huu, tunakumbushwa kuhusu uzalendo, umoja, na dhamira yetu ya kujenga taifa imara lenye maendeleo.

Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali watendaji wa taasisi za Serikali viongozi wa dini na Naibu Katibu wa Maliasili na Utalii anayeshughulikia eneo la Utalii Nkoba Eliezer Mabula.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here