Watumishi madini watakiwa kuweka mazingira mazuri ya kuvutia wawekezaji

0

Asteria Muhozya na Tito Mselem, Morogoro

WATUMISHI wa Wizara ya Madini na Taasisi zake wametakiwa kuweka mazingira wezeshi kwenye maeneo yao ya kazi yatakayovutia uwekezaji katika sekta ya Madini ili hatimaye Serikali iweze kunufaika na kupata mapato stahiki yanayotokana na rasilimali Madini.

Hayo yameleezwa na Katibu Mkuu Wizara ya Madini Adolf Nduguru kwa niaba ya Waziri wa Madini wakati akifungua mkutano wa Baraza la Wafanyakazi uliofanyika mkoani Morogoro na kutanguliwa na  mkutano wa mafunzo  kwa wajumbe wa baraza hilo.

Aliongeza, kwa kufanya hivyo kutaiwezesha sekta ya Madini kuongeza mchango wake katika Pato la Taifa  na kufikia mchango wa asilimia 10 ifikapo mwaka 2022 kama ilivyo ainishwa katika Dira ya Maendeleo ya Taifa.

Alisema, ili kufikia asilimia hiyo ni lazima wawepo wawekezaji na kwamba lengo hilo litafikiwa kikamilifu kwa watumishi kuhakikisha wanaweka mazingira wezeshi katika maeneo yao ya kazi  ikiwemo kuhakikisha huduma wezeshi za kiuwekezaji zinatolewa, leseni zinatolewa,  pamoja na mazingira mengine ambayo yatawezesha kutoa matokeo mazuri  na hivyo  kuchochea uwekezaji zaidi.

“Sheria ya Madini iko wazi, wawekezaji siyo wahisani, kama tunavyojua Serikali inapata mapato yake kupitia kodi na mirabaha. Aidha, kwenye uwekezaji mkubwa na wa kati kama serikali tuna hisa za asilimia 16 ambazo hazipungui thamani,’’ alisisitiza Katibu Mkuu Nduguru.

Pia, Nduguru alisema kama watumishi wa umma, wanao wajibu wa kutekeleza majukumu yao na kusimamia sekta ya Madini kwa uzalendo, weledi, uaminifu na ufanisi ili kutimiza matarajio ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Hassan ya kuona sekta ya Madini inalinufaisha Taifa na watanzania kutokana na rasilimali ambazo nchi imejaaliwa kuwa nazo.

Nduguru alisema, kushiriki katika mkutano huo, kunatoa fursa ya kujitathmini na kupima mwenendo wa utekelezaji wa majukumu baada ya kutekeleza bajeti katika robo ya kwanza ya mwaka 2022/23.

Akisoma risala fupi Katibu wa  Chama Cha Watumishi wa Serikali Kuu na Afya (TUGHE) Tawi la Wizara ya Madini Cecilia Mrope ameipongeza wizara kutokana na mafanikio kadhaa yaliyopatikana na kuiomba wizara  kuona umuhimu wa kuwakutanisha wataalam wa wizara na taasisi ili kujadili masuala makubwa yatakayoiwezesha wizara kuongeza migodi, mapato, kubuni miradi chochevu na kukwamua iwaipo miradi iliyokwama kuanza.  

Awali, Mjumbe wa TUGHE kutoka Makao Makuu Taifa Dennis Tosiri ameipongeza wizara ya madini kutokana na namna inavyoshughulikia changamoto za watumishi na kuongeza kuwa, kutekelezwa kwa changamoto hizo katika maeneo yao kunasaidia kuongeza tija na ufanisi wa kazi.

Pia, ametaka Tughe tawi la wizara kuhakikisha linaongeza idadi ya wanachama na kueleza kwamba suala hilo  litakiwezesha  chama kuwa  imara na kusaidia   masuala mengine kuendelea.

Katika Mkutano  huo, wajumbe wa baraza wamepata fursa ya  kupokea taarifa mbalimbali za utekelezaji wa majukumu ya wizara  ikiwemo taarifa ya matumizi na mwenendo wa matumizi ya Bajeti kwa robo ya kwanza ya Mwaka wa Fedha 2022/23 na taarifa nyingine.

Aidha, katika mkutano huo, wizara imetumia kutoa vyeti vya kutambua mchango wa watumishi kadhaa wa wizara  waliostaafu na ambao wanatarajia kustaafu kwa mujibu wa Sheria  katika kipindi cha mwaka 2022/23.

Vilevile, wizara imetumia nafasi hiyo kumpongeza mtumishi wa wizara Nyamwiza Ndibalema ambaye alipata medali tatu moja ikiwa ya dhahabu na mbili za shaba kutokana na kushinda mbio za mita 3,000,  1500 na mita 800 katika mashindano ya  Shirikisho la Michezo la Wizara, Taasisi na Idara za Serikali (SHIMIWI) yaliyofanyika hivi karibuni mkoani Tanga.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here