Na Mwandishi Wetu
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Zanzibar Nuru Foundation Mama Zainab Kombo Shaib, ameikumbusha jamii kuondoa dhana kwamba watoto yatima ni mzigo na lazima kutambua kwamba, upo wajibu wa kuwalea kwa pamoja na kuwapa kila aina ya matunzo wanayostahiki ikiwemo elimu.
Mama Zainab ambaye pia ni Mke wa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar ameyasema hayo huko Donge Mchangani Kaskazini ‘A’ Unguja alipokuwa akigawa msaada chakula kwa watoto yatima na wanawake wanaoishi katika Mazingira Magumu wilayani humo.
Amefahamisha kwamba, kufanya hivyo ni hatua muhimu ya kuwafanya watoto waliofiwa na wazazi wao kuishi kwa furaha na kuendelea kupata matunzo na huduma mbali mbali kutoka kwa jamiii.
Alisema, Jumuiya ya Nuru Foundation inayojishughulisha na kuwasaidia mayatima na wanawake walio kwenye mazingira magumu na kwamba pia ni wajibu wa kila mmoja katika jamii kutimiza wajibu wa kuelimishana katika kuwatunza na kuthamini watoto mayatima.
Mama Zainab amewataka wazazi na walezi wenye watoto mayatima kuhakikisha kwamba hawabaki nao majumbani kimya kimya na badala yake kuwasajili na kuwatolea taarifa zao kwa usahihi katika Taasisi na Jumuiya za namna hiyo ili iwe rahisi kuwapatiwa misaada ya mahitaji yao.
Ameonya tabia ya baadhi ya wanawake kujisahau na kuwapa manyanyaso watoto yatima baadala ya kuwapatia haki zao ikiwemo elimu, makazi na nyenginezo za msingi ili maisha yao yaweze kuwa bora.
Naye Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar Riziki Pembe Juma alisema watoto mayatima ni kundi kubwa lililopo ndani ya jamii linalohitaji kusaidiwa hivyo Jumuiya ya Nuru Foundation inafanya jambo jema kuisaidia Serikali katika kuwapatia huduma watoto wa aina hiyo.
Amefahamisha kwamba, hatua ya kuwasaidia watoto hao ni muhimu kuendelea kufanyika kwa kuwa ni kuunga mkono juhudi za Serikali kwa vile pekee haiwezi kufanya kila kitu.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na watoto Abeda Rashid Abdalla, amesema kwamba shughuli za taasisi kama Nuru Foundation ni muhimu hasa katika kuwasaidia kuwapunguzia mzigo wanawake ambao ndio wanaobeba jukumu kubwa la kuwalea mayatima.
Kwa upande wake Mratibu wa Watoto mayatima wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Mwajuma Kali Makame ameshukuru ujio wa Viongozi wa Jumiya hiyo ulioambatana na Uongozi wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia na watoto na kusema kwamba inatoa fikra mpya katika kuendelea na jitihada za pamoja ya kuwatunza na kuwalea watoto yatima na wanawake wenye mazingira magumu.