Wandamba wazindua kitabu cha historia

0

Na Winfrida Mtoi

KATIKA kuhakikisha asili ya kabila la kindamba inajulikana zaidi, watafiti wa lugha ya kabila hilo wameungana na kuandika kitabu kilichoelezea historia nzima na maisha ya Wandamba.

Kitabu hicho kilichozinduliwa hivi karibuni, jijini Dar es Salaam, kimeandikwa kwa ushirikiano wa watu watano ambao wanatokea katika kabila hilo la Mkoani Morogoro.

Waandishi wa kitabu hicho ni Padri Fidelis Mfalanyombo, Agathon Kipandula, John Chilipwel, Asernius Ndege na Leoni Mbala ambao wote ni wazaliwa wa mkoa huo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakati wa uzinduzi wa kitabu hicho, walisema lengo la kuandika kitabu hicho ni kulifanya kabila hilo dogo kujulikana na kuwasaidia vijana wa kutambua asili na chimbuko la kabila lao.

Padri Mfalanyombo ambaye alianza kufanya utafiti wa kabila hilo tangu mwaka 2002, alisema alipata msukumo wa kuandika kitabu hicho ili kuweka historia kuwa Wandamba wana kitabu, lakini pia baada ya kuona makabila mengine kama Wangoni wana kitabu chao.

“Katika kitabu hiki kuna historia ya Wandamba na asili yao, utawala, jinsi walivyokuwa wanapata elimu, maisha, makazi wanayopenda kuishi, sherehe, dawa, ndoa na taratibu za majina,” alifafanua Padre Mfalanyombo.

Alisema, kitabu hicho kwa sasa kinapatikana katika lugha ya kiswahili, lakini ameanza kukitafsiri kwa Kiingereza ili watu wengi zaidi hata wageni waweze kuisoma historia ya kabila hilo.

Naye Kipandula ambaye ni mwandishi na mtafiti wa lugha, alieleza kuwa, kabla ya kutoa kitabu hicho alishaandika kamusi mbili za lugha ya kabila hilo, ndipo alipopata wazo la kitabu.

Kwa upande wake Chilipwel alieleza kwa ufupi sababu ya kabila hilo kutojulikana kama ilivyo kwa makabila mengine ya Morogoro, ni kwamba hawakupenda kuwa watumwa wa wakoloni, wala kulipa kodi ya kichwa iliyokuwepo zamani.

“Wandamba ni kabila dogo, lakini wana tabia moja ambayo hawapendi kutumwa, Wapogoro walijulikana zaidi kwa sababu walikuwa wanapenda kufanya kazi za wakoloni, walitangulia kufika Dar es Salaam tofauti na sisi,” alisimulia Chilipwel.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here