Wananchi Mbwamaji wamtuma Mwenyekiti wao kwa Rais Samia

0

Na Mwandishi Wetu, Kigamboni

WANANCHI wa Mtaa wa Mbwamaji Geza ulole uliopo Kata ya Somangila, Wilaya ya Kigamboni wamemuomba Mwenyekiti wa Mtaa huo Yohana Luhemeja kufikisha maombi ya changamoto za Mtaa huo kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.

Wananchi hao wametoa rai hiyo katika mkutano wa hadhara uliofanyika mwishoni mwa wiki ulioitishwa na Mwenyekiti huyo, uliokuwa na ajenda mbalimbali ikiwemo ajenda kuu ya ukosefu wa Shule ya Msingi Mtaa wa Mbwamaji.

Ajenda nyingine ni uboreshaji wa Miundombinu ya barabara, usafi wa mazingira, Ulinzi na Usalama, umaliziaji wa upimaji shirikishi (Ardhi) na ukarabati wa jengo la Serikali ya Mtaa.

Wananchi hao walipaza sauti juu ya kuboreshwa miundombinu ya barabara kwa kuwa barabara zote za mtaa ni mbovu na tangu 2014 hadi sasa, hakuna barabara iliyo tengenezwa kwa kiwango cha changarawe, licha ya kuwasilisha maombi yao mara kadhaa kwa Mkurugenzi, ila hakuna mafanikio.

Wamesema Serikali imewasahau wananchi wa mtaa wa Mbwamaji Geza ulole, kwani hata kwenye ilani ya CCM, hakuna mradi hata mmoja waliopewa.

Wananchi hao, wamebainisha kero hizo zimekuwapo muda mrefu, hivyo wameomba Mwenyekiti huyo mpya aweze kuzitatua huku zile kubwa aziwasilishe kwa Rais Samia.

Mbali na kuwasilisha changamoto hizo, wananchi hao wamempongeza Mwenyekiti wao Yohana Luhemeja kwa kuitisha mkutano huo, kwani imekuwa tofauti na iongozi uliopita 2019 hadi 2024 ambao hawakuitisha mkutano wa wananchi.

Naye, Mwenyekiti Luhemeja akijibu kero hizo za Wananchi, alisema: “Masuala kama Shule, Mtaro, Barabara tayari nilisha wasilisha kwenye kamati ya Maendeleo ya Kata pia Ofisi ya Mtaa, tulishaandika barua kwa Mkurugenzi tunasubiri majibu. Nina hakika Rais wetu ni msikivu watayafanyia kazi kupitia watendaji wake wanaomsaidia katika ngazi zote.”

Aidha, Luhemeja amebainisha kuwa, awali shule ya Msingi mtaa wa Mbwamaji hapo awali ulikuwa na shule ya Msingi Geza Ulole iliyo hamishiwa Mtaa wa Kizani kwa kupisha eneo hilo ambalo linatarajiwa kujengwa soko/kiwanda cha samaki.

Hata hivyo, wananchi wamesema, mabadiliko hayo hawakushirikishwa pamoja na hayo wananchi wamerudia tena ombi la kujengwa shule mpya kwenye eneo walilolipitisha ndani ya Mtaa huo wa Mbwamaji.

Mtaa huo una wanafunzi zaidi ya 750 ambao wanasoma nje ya mtaa huo, hali inayopelekea watoto kupata shida hasa wakati wa masika.

Mbwamaji Geza ulole ni miongoni mwa mitaa kongowe nchini yenye kubeba historia Dar es Salaam.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here