Na Mwandishi Wetu
KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis amesema, wananchi wa Bumbwini, Mkoa wa Kaskazini Unguja wameweka wazi kwamba hawamdai Rais Dkt. Hussein Mwinyi.
Mbeto alisema hayo kwenye mkutano wa kampeni, uliofanyika jana Oktoba 3, 2025, kwenye uwanja wa michezo wa Bumbwini Kidimni wakati akifikisha salamu za wazee ambao wamekiri kufikiwa na maendeleo yanayofanywa na Rais Mwinyi, hivyo wamemuhakikishia watamchagua tena mgombea huyo wa CCM kwenye Uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 29, 2025.
Mwenezi huyo alisema, baada ya kufika Bumbwini alizungumza na wazee hao ambao walimtajia mambo ambayo yamefanyika katika kipindi cha miaka mitano ya Rais Mwinyi ikiwemo ujenzi wa barabara sita, ghorofa maeneo ya Misufini na Makoba, pia wana tanki la maji. “Wamesema wana hospitali ya Wilaya, wana barabara ya mita 60.”
Mbeto alisema, licha ya wananchi kuyaona yote hayo kwa macho, wapinzani wamekuwa wakibeza jitihada hizo zinazofanywa na Dkt. Mwinyi, huku wao wakishindwa kuweka wazi watakayoyafanya iwapo watapewa ridhaa ya kushika dola.
Alisema, jambo pekee ambalo wamekuwa wakilifanya wapinzania kwenye majukwaa yao ya kampeni, ni kutoa matusi sambamba na kuiga yale yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Nane.
Aidha, Mbeto alitumia nafasi hiyo kumsihi Dkt. Mwinyi kuendelea kuwaletea Wazanzibar maendeleo, kwani yeye ni mti wenye matunda, hivyo ni lazima apopolewe.
“Mti wenye matunda ndio unaopopolewa mawe. Dkt. Mwinyi ni mti wenye matunda, acha watu wakupopoe mawe angalau wapate matunda waongeze uhai wao,” alisema Mbeto.