Wanamichezo watakiwa kuiletea nchi heshima

0

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa wanamichezo kushiriki mashindano ya Jumuiya ya Madola kama washindani wa kweli ambao wataonesha vipaji na kuiletea Tanzania heshima.

Makamu wa Rais ametoa wito huo wakati akipokea Kifimbo cha Mfalme wa Uingereza kuelekea Mashindano ya Michezo ya Jumuiya ya Madola itakayofanyika Glasgow Uingereza mwaka 2026.

Amesisitiza umuhimu wa taasisi na mashirikisho ya michezo kuibua, kukuza na kuwezesha vipaji hasa miongoni mwa vijana wanaobeba matumaini ya Taifa.

Pia, Makamu wa Rais ametoa rai kwa wadau wote, wakiwemo wakala wa Serikali, mashirikisho ya michezo, wadau wa maendeleo na sekta binafsi kuungana pamoja kwa ushirikiano wa kimkakati ili kuhakikisha wanamichezo wa Tanzania wanapewa mafunzo, nyenzo na msaada wa kisaikolojia unaohitajika.

Alisema, ni muhimu kutambua kwamba Michezo ya Jumuiya ya Madola ni zaidi ya tukio la kimichezo kwa kuwa ni sherehe ya historia ya pamoja, maadili, na ushirikiano kati ya mataifa wanachama ambayo yanaunganishwa na historia ya pamoja na ahadi ya kudumu ya amani, demokrasia na maendeleo endelevu.

Halikadhalika Makamu wa Rais alisema kuwasili kwa Kifimbo cha Mfalme wa Uingereza ambacho kinabeba ujumbe wa uhifadhi wa mazingira hususani udhibiti wa taka za plastiki baharini kunapaswa kuikumbusha jamii wito wa kuchukua hatua na kuwajibika katika kutunza mazingira.

Alisema, Kifimbo hicho kinatoa fursa ya kutafakari juu ya umuhimu wa maandalizi ya mapema, ya kina na yanayoratibiwa vema katika kuelekea katika Michezo ya Jumuiya ya Madola ya 2026 huko Glasgow.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Gerson Msigwa alisema, Wizara kwa kushirikiana na kamati ya olimpiki imeweka mpango mkakati wa kuanza maandalizi mapema ili kushiriki vema mashindano ya Jumuiya ya Madola.

Alisema, ipo fursa kubwa ya kupata medali nyingi zaidi hivyo maandalizi ya mapema yatafanyika ili kuandaa vijana katika michezo yote.

Msigwa alisema, Serikali inawekeza kwa kiasi kikubwa katika michezo na kujenga miundombinu ikiwemo ujenzi wa mradi mkubwa wa kuendeleza michezo kama vile ujenzi wa kituo cha kuwawezesha wanamichezo wanaoshiriki Jumuiya ya Madola na Olimpiki mjini Babati.

Aliongeza, lengo la ujenzi wa kituo hicho mjini Babati ni kuhakikisha wanamichezo wanafanya maandalizi katika hali ya hewa rafiki kuendana na maeneo mengine Duniani yanakofanyika mashindano hayo.

Makamu wa Rais alipokea Kifimbo cha Mfalme wa Uingereza ambacho kilimaliza muda wake nchini Cameroon na amekabidhi Kifimbo hicho ili kiweze kuelekea nchini Ghana.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here