Wakuu wa nchi za SADC kukutana kwa dharura Angola

0

Na Mwandishi Wetu


WAKUU wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wanatarajia kukutana katika mkutano wa dharura Jijini Luanda, Angola, Novemba 4, 2023.

Mkutano huo unalenga kujadili juhudi za SADC katika kuimarisha hali ya amani, ulinzi na usalama Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kufuatia mapigano ya muda mrefu yanayoendelea nchini humo yakitekelezwa na vikundi vyenye silaha katika majimbo ya Kivu Kusini, Kivu Kaskazini na Ituri.

Katika Mkutano huo ujumbe wa Tanzania unatarajiwa kuongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ataambatana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba, pamoja na Maafisa Waandamizi wa Serikali.

Pamoja na masuala mengine, mkutano huo unatarajiwa kusisitiza umuhimu wa utashi wa kisiasa kwa Nchi Wanachama katika kuchangia askari na vifaa vya kijeshi kwa ajili ya Misheni ya Ulinzi wa Amani ya SADC nchini DRC (SAMIDRC), ambapo hadi sasa nchi tatu pekee ndizo zimechangia askari na vifaa vya kijeshi katika misheni hiyo. Nchi hizo ni Tanzania, Afrika Kusini na Malawi.

Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali utatanguliwa na mkutano wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama na Kikao cha Kamati ya Kudumu ya Makatibu Wakuu na Mawaziri vitakavyofanyika Novemba 3, 2023.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here