Wakandarasi wazawa kuneemeka miradi ya usambazaji umeme nchini

0
Waziri wa Nishati Januari Makamba.

Na Mwandishi Wetu

WAZIRI wa Nishati Januari Makamba amesema, Serikali inatarajia kuwapa kipaumbele wakandarasi wazawa na wadogo kwenye miradi mbalimbali ya usambazaji umeme nchini inayosimamiwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

Mbali na miradi hiyo ambayo inaendelea kutekelezwa, mradi mwingine ambao unatarajia kutoa fursa kwa wakandarasi wa ndani, ni usambazaji umeme vitongojini ambao unatarajia kugharimu Shilingi zaidi ya Trilioni 6.

Akizungumza kwenye kikao kilichowakutanisha Wajumbe wa Bodi ya Nishati Vijijini, Wataalamu kutoka REA, TANESCO, Wizarani na wakandarasi wanaotekeleza miradi ya usambazaji umeme, kilichofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam, Waziri Makamba alisema, kwasasa wanataka kuwapa kazi wakandarasi ambao wanatekeleza vizuri wajibu wao.

“Ndani ya miezi ijayo tutazindua programu ya umeme vitongojini, huu ni mpango mkubwa sana kwa nchi yetu, hatuwezi kwenda na watu ambao hawapo ‘serious,’ hii biashara ya kusambaza umeme ni kubwa sana, na kazi ya kusambaza umeme vijijini ndio kwanza inaanza, mna fursa kubwa ya kupata fedha nyingi sana na kukuza kampuni zenu,” alisema Waziri Makamba.

Alisema, fursa hiyo kwa kiasi kikubwa wanataka kuwapa wakandarasi wa ndani, ila itategemea na utendaji wao kwenye kazi ambazo wanaendelea kuzifanya kwenye maeneo mbalimbali, na kama watasuasua, fursa hiyo itapelekwa kwa kampuni kubwa za nje ya nchi.

“Hii fursa tunataka iende kwa wakandarasi wa ndani, ila wakishindwa, hatutasita kuwapa wakandarasi wakubwa duniani, mliobaki mtakuwa sub-contractors au mtakaa pembeni, tunataka wakandarasi wakubwa na wadogo wachukue kazi za REA ili wakue,” alisema.

Waziri Makamba alisema, kazi ya REA sio kuwalea wakandarasi wazawa, bali ni kuwapa kazi ambazo zitawasaidia kukua “kuna wakandarasi wadogo ambao wana ari na wanataka kufanya kazi, hii kazi haiwezi kuwa ya watu wachache, tutawapa na wengine.”

Hata hivyo, Waziri Makamba alisema, ili wakandarasi wanaotekeleza miradi ya umeme hivi sasa wawepo kwenye orodha ya kusambaza umeme vitongojini na miradi mingine inayokuja, wanapaswa kukamilisha kazi walizopewa, “nawapa miezi miwili kabla ya mfumo mpya haujaanza, ni muda wa kuchakarika na kumaliza kazi ili muweze kubaki kwenye orodha.”

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here