Wajasiriamali Zanzibar kuboreshewa mazingira

0

MGOMBEA wa nafasi ya Rais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya biashara kwa kuhakikisha wajasiriamali wanafanya shughuli zao kwa utulivu na katika maeneo bora zaidi.

Akizungumza katika mkutano na makundi ya wajasiriamali uliofanyika katika Ukumbi wa Idrisa Abdulwakil, Kikwajuni, Mkoa wa Mjini Magharibi leo Oktoba 9, 2025, Dkt. Mwinyi amesema Serikali imejipanga kutatua changamoto zinazowakabili wajasiriamali wengi, hasa wanawake.

Aidha, Dkt.Mwinyi ameeleza kuwa Serikali ilitenga Shilingi Bilioni 96 kwa ajili ya kuwawezesha wajasiriamali nchini, lakini baadhi yao hawakufikiwa, hivyo katika awamu ijayo Serikali itaweka utaratibu bora zaidi kuhakikisha fedha hizo zinawafikia walengwa wote.

Halikadhalika, Dkt. Mwinyi ameagiza Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar (ZEEA) kuwapatia wajasiriamali mafunzo kabla ya kutoa mikopo, ili fedha wanazopata ziwe na tija na ziweze kuwainua kiuchumi.

Vilevile, ameeleza kuwa Serikali itaendelea kutenga fedha za mitaji na kuwafikia wajasiriamali katika maeneo yao, sambamba na kurahisisha upatikanaji wa mikopo midogo midogo kwa ajili ya kuboresha biashara zao.

Kuhusu masoko, Dkt. Mwinyi amesema Serikali itashirikiana na wawekezaji, hasa katika sekta ya utalii, ili kuhakikisha bidhaa za wajasiriamali zinaingia katika masoko ya hoteli na maeneo mengine ya kitalii.

Dkt.Mwinyi amesema Serikali itatenga fedha kwa ajili ya kuanzisha viwanda vidogo vidogo, vitakavyowaajiri wananchi wengi zaidi, na kusaidia kuongeza thamani ya bidhaa zinazozalishwa na wajasiriamali.

Akizungumzia miradi mikubwa ya maendeleo, Dkt. Mwinyi amebainisha kuwa Mradi wa BIG Z unalenga kujenga vibanda vya kisasa pembezoni mwa barabara za mjini, kwa ajili ya wajasiriamali kufanya biashara zao katika mazingira salama na yenye heshima.

Dkt. Mwinyi ametumia fursa hiyo kuwahamasisha wajasiriamali na wananchi kwa ujumla kujitokeza kwa wingi kupiga kura na kuwachagua wagombea wa CCM, ili Serikali iendelee kuleta maendeleo makubwa zaidi kwa wananchi wote wa Zanzibar.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here