Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Mhandisi Hamad Yussuf Masauni
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Mhandisi Hamad Yussuf Masauni amewataka Wahariri na Waandishi wa vyombo vya habari kuacha ushabiki wa watu binafsi na kuepuka kuandika na kusambaza habari zenye ushawishi wa uvunjifu wa amani, kwa kuzingatia maadili yao kwa lengo la kulinda maslahi ya taifa.
Ameyasema hayo wakati alipofungua Semina ya Wahariri wa Vyombo vya habari Zanzibar huko ZURA Maisara Mkoa wa Mjini Magharibi amesema kudumisha amani na umoja wa wananchi ni muhimu kwa maslahi ya vizazi vya sasa na vya baadae.
Aidha, amesema kuwa msingi mkuu wa amani na utulivu wa taifa uliopo nchini ni Muungano, ambao umeendelea kuimarisha umoja, mshikamano na maendeleo ya Watanzania.
Hatahivyo Masauni amefafanua kua ni wajibu kwa Wanahabari kutoa elimu kwa jamii kwa kutoa historia, Katiba na sheria za Muungano ili wananchi waweze kujua wapi tulipotoka na wapi Nchi inaelekea kwa kudumisha Amani iliyopo ya Muungano.
Vilevile amewasisitiza kuiga misingi mizuri iliyoanzishwa na waasisi wa Muungano kwani hawakujali kitu wala kuwa na tamaa na kuviweka karibu visiwa viwili vya unguja na pemba kua pamoja na Tanzania.
Nae Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Sera Uratibu wa Baraza la wawakilishi Hamza Hassan Juma amesema Wanahabari ni vyema kuelezea vizuri muungano kwa jamii kwani asilimia 70 ya wananchi wamezaliwa baada ya Muungano na nchi imekuwa kama kijiji kupitia mitandao ya kijamii.
Aidha, amewataka wanahabari kuitumia nafasi ya kuenzi na kùlinda Muungano kwani waasisi wetu wameungana bila ya kulazimishana, hivyo ni wajibu wa wanahabari kutumia kalamu zao kwa kuelimisha umma juu ya Muungano
“Tuitumie vizuri nafasi hii ya kulinda na kudumisha Muungano wetu kwani wazee wetu wameungana bila ya kulazimishana kwa kuona umuhimu wa jambo hili na sisi tuendelee na wao na tuepuke kufuata matakwa ya watu binafsi kuhusu Muungano wetu.
Akitoa mada juu ya upekee wa Muungano wetu Dkt Abdalla Mkumbukwa amesema muungano wetu unamuundo wa kipekee ambao haupo popote duniani kutokana na muundo wa sheria za nchi.
Ameongezea kuwa Muungano huo umedumu kwa kipindi cha miaka 61 hadi sasa kwani kunabaadi ya nchi baada ya kupata Uhuru wameungana na imeshavunjika kutokana na changamoto zilizomo ikiwemo Misri na Syria, Senegal na Zambia.
“Huu ni Muungano uliodumu kwa nchi za Afrika kwani nchi nyinyi baada ya kupata uhuru waliungana lakini wameuvunja muungano huo kutokana na changamoto zilizomo katika nchi zao kama vile Misri na Syria na Senegal na Zambia,” amesema Dkt. Abdalla.
Nae, Dkt. Harrison Mwakyembe akitoa mada kuhusu Muungano chimbuko misingi na fursa za Muungano amesema, Muungano ndio unaoleta fursa mbalimbali za kiuchumi na kijamii, hivyo ni vyema kuuendeleza kwa maslahi ya nchi.
Aidha, amesema nchi yetu imepata uhuru mnamo miaka ya 20 kwa kuanzisha taasisi mbalimbali na kuweza kupanga mikakati ili kupambana na wakoloni kwa kuweza kupata uhuru na hadi sasa nchi imeendelea na kuwa na uchumi mkubwa kwa Afrika mashariki.
Semina hiyo ya siku moja ambayo imewashirikisha Wahariri, Waandishi wa habari Wadau mbalimbali wa Habari kutoka Zanzibar na Tanzania bara na mada 3 zimejadiliwa katika Semina hiyo ambazo ni Muungano, Chimbuko,Misingi na Fursa za Muungano, upekee wa Muungano na Wajibu wa Wahariri wa Vyombo vya habari katika kulinda na kuenzi Muungano.