Wadau wa elimu watoa msaada wa sare za shule Kibaha DC

0

HALMASHAURI ya Wilaya ya Kibaha imepokea msaada wa sare za shule, viatu, soksi na mabegi kutoka kwa wadau wa elimu, ukilenga kuwasaidia wanafunzi kutoka familia zenye mazingira magumu katika shule saba za msingi zilizoko kwenye kata za Magindu na Gwata.

Msaada huo umetolewa na asasi ya kiraia DIDO Mwanafunzi Initiative yenye Makao yake Makuu Bunju, Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya jitihada zake za kuchochea maendeleo ya elimu katika maeneo ya vijijini.

Jumla ya sare 2,000, mabegi 200, soksi 200 na jozi 200 za viatu vimetolewa kwa wanafunzi wa shule za msingi Umoja, Ngwale, Gwata, Gumba, Magindu, Lukenge na Miyombo.

Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano iliyofanyika katika Kata ya Magindu, Afisa Elimu Msingi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha, Bernadina Kahabuka, aliishukuru taasisi hiyo kwa moyo wa upendo waliouonesha kwa watoto wa Kitanzania, hususan walioko katika mazingira magumu.

“Msaada huu umekuja kwa wakati muafaka. Utaongeza ari ya kujifunza, kupunguza utoro na hatimaye kuinua ufaulu wa wanafunzi wetu,” alisema Kahabuka.

Aidha, aliwataka wanafunzi waliopokea msaada huo kuzitunza sare hizo na kuziona kama kichocheo cha kuongeza bidii katika masomo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa DIDO Mwanafunzi Initiative, Rehema Moses, alisema mchango huo ni sehemu ya dhamira ya taasisi yake ya kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuinua sekta ya elimu.

“Tunatambua changamoto zinazowakabili watoto kutoka familia zisizo na uwezo. Huu ni mchango wetu katika kuleta usawa wa kielimu na kuwatia moyo wanafunzi kutimiza ndoto zao,” alisema Rehema.

Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Gumba, Moses Yusuph, aliwashukuru wadau hao na Halmashauri kwa kutambua umuhimu wa kusaidia shule zilizoko pembezoni na wanafunzi wanaoishi katika mazingira magumu, akisema hatua hiyo inaongeza matumaini na hamasa kwa jamii.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here