Waajiri wasiowasilisha michango PSSSF na NSSF kubanwa

0
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Prof. Joyce Ndalichako.

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Prof. Joyce Ndalichako amesema Kamati Maalum imeundwa kwa ajili ya kufuatilia fedha za michango ya wanachama wa Mfuko ya Hifadhi ya Jamii PSSSF na NSSF ambazo hazijawasilishwa na waajiri.

Akichangia bungeni taarifa ya Kamati za bunge zinazoshughulikia ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Prof. Ndalichako alisema, katika ripoti ya CAG mfuko huo ulikuwa ukidai michango Shilingi Bilioni 408 ambazo zilikuwa hazijakusanywa baada ya maelekezo ya Rais na kuzingatia hoja za CAG iliundwa Kamati hiyo.

Alisema, Kamati hiyo imefanikiwa kukusanya Shilingi Bilioni 200.6 kati ya Shilingi Bilioni 408 na kusisitiza Serikali itahakikisha fedha zilizobaki zinakusanywa.

Kuhusu michango ya wafanyakazi wa halmashauri, Profesa Ndalichako alisema kiliundwa kikosi kazi Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) na tayari wameingia makubaliano na halmashauri 81 ambazo zina madai ya muda mrefu na zimewesha kuwakomboa wastaafu 1,425 kulipwa madai yao.

Aidha, Waziri Ndalichako amemuagiza Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF kufuatilia Halmashauri 103 ambazo hazijaweka makubaliano namna watakavyowasilisha michango wanayodaiwa kwa muda mrefu.

“Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI nitakukabidhi orodha ya Halmashauri ili fedha hizo zikusanywe tuweze kulipa mafao wastaafu wetu,” alisema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here