Vyama vya upinzani vina jambo la kujifunza kabla ya Oktoba 2025

0

ZOEZI la uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa mwaka 2024 lilihitimishwa rasmi kwa Chama cha Mapinduzi (CCM) kushinda kwa zaidi ya asilimia 98 kila kiti na upinzani kushinda kwa chini ya asilimia moja nchi nzima.

Tathmini inaonesha kuwa, vyama vya upinzani pamoja na changamoto za hapa na pale zilizojitokeza bila kuathiri zoezi zima la uchaguzi, havijajipanga na visipoangalia mwaka ujao 2025 vitajifuta vyenyewe katika ulingo wa siasa nchini.

Kabla ya tathmini yangu pevu katika makala hii, naomba ieleweke kuwa dosari zilizojitokeza katika uchaguzi ulioisha zilikuwa ndogo ambazo hazikuathiri zoezi hilo.

Duniani hakuna nchi yoyote ambayo inafanya uchaguzi ambao hauna dosari hata nchi zilizoendelea kama Marekani tumeshuhudia juzi tu Rais Mteule, Donald Trump akinusurika mara mbili kuuawa wakati wa kampeni. Ikumbukwe Marekani ndio nchi ambayo miaka yote imekuwa kioo cha demokrasia duniani.

Zipo nchi kama Georgia, Uingereza, Ufaransa na nyingine nyingi ambazo zimekumbwa na dosari nyingi kipindi cha kampeni za uchaguzi, lakini dosari hizo hazikuathiri zoezi la upigaji kura na washindi wamepatikana.

Tofauti na vyama vya upinzani vya hapa nchini. Marekani mpinzani kama Donald Trump na chama chake cha Republican wameshinda chama tawala cha Democrat kwa kuwa walikuwa wamejipanga.

Na hapa ndo hoja zangu zinaanzia kuwa, upinzani umeangukia pua Tanzania kwa sababu ulikuwa haukujipanga kushinda uchaguzi. Hizi ni sababu chache za upinzani kushindwa:

Ukosefu wa timu za ushauri ndani ya vyama (Think tanks).

Ukiangalia vyama vya upinzani karibia vyote nchini havina timu nzuri na bobevu kama vilivyokuwa zamani. Chukulia mfano kama CHADEMA kipindi kile kikiwa na uongozi imara na timu ya watu wabobevu kama marehemu Profesa Mwesiga Baregu, Profesa Safari na wengineo chama kilikuwa kinatembea katika mwelekeo wa sahihi, ndo maana enzi hizo CHADEMA kilikuwa kinashinda viti vingi nchi nzima na kuleta upinzani wa kweli kwa CCM. Kwa sasa CHADEMA inayumba kama debe tupu viongozi wake hawana mwelekeo.

Ukosefu wa Mipango thabiti ya ushindi

Kawaida na kitaalamu uchaguzi ukiisha ndo mwanzo wa maandalizi ya uchaguzi unaofuata. Sasa vyama vikubwa kama CHADEMA vilijitoa katika uchaguzi wa Serikali za mitaa wa mwaka 2019, hivyo wakawa nje ya Serikali na mfumo na kwa mantiki hii hawakujiandalia uchaguzi wa mwaka huu. Hivyo katika uchaguzi huu walikuwa kama wageni wapya katika nyumba mpya.

Migongano na mizozo ndani ya vyama

Vyama vya upinzani karibia vyote vimekuwa katika mizizo na migawanyiko tangu uchaguzi uliopita kitu ambacho kimevifanya kutokuwa na umoja na mshikakamamo kwa wao na wananchi wao. Chama kama CHADEMA kimegombana na wanachama na viongozi wake mpaka siku wanaingia katika uchaguzi wa serikali za mitaa.

Ukata wa fedha

Siku zote mtaji wa chama ni wanachama na rasilimali fedha. Na chama kwa nchi kama yetu mapato yake ya kwanza ni ruzuku kulingana na viongozi ulio nao ndani ya Serikali. Chama kama CHADEMA kilijitoa katika uchaguzi wa mwaka 2019 hivyo hakikuwa na ruzuku. Hata wafadhili wake wake nje na ndani walipunguza misaada yao ya pesa kwa sababu ya chama kukosa mvuto. Ikumbukwe pesa uwekezwa pale penye njia na mvuto.

Hadaa na usaliti wa Viongozi wa upinzani kwa Wananchi

Usaliti wa viongozi wa upinzani kwa wananchi umesabababisha wananchi kukosa imani navyo. Mfano mzuri na halisi ni Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, huyu aliwasaliti na kuwaadaa wanaChadema kuingia katika kampeini kumbe hakujiandikisha kupiga kura. Kiongozi lazima uwe mfano kwa unaowaongoza sasa adaa kama za Lissu ni mwananchi yupi atamuamini na kuamini chama chake?

Miongozo ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa


Kwenye hili nikipongeze chama cha ACT Wazalendo ndo chama pekee cha upinzani kilichotoa mwongozo wa uchaguzi kwa wanachama wake. Na huu mwongozo umekisaidia kushinda nafasi ya tatu Kitaifa. CCM sababu ya uzoefu wake katika medali za siasa, kilihakikisha kinatoa mwongozo mapema kwa wanachama wake mpaka mchakato wa uchaguzi unaanza wanaccm walikuwa wanajua nini wafanye.

Hatima ya vyama vya upinzani mwaka 2025

Iwapo upinzani hautajisahihisha na kuacha ubinafsi mwaka 2025, utapotea kabisa na hautapata wabunge na madiwani. Kwa sasa, hivi vyama vikubwa kama CHADEMA vimekosa mvuto, hivyo vinahitaji kuvuka maji ya tanga; yaani kujisahihisha ili viendelee kuwa katika ramani ya upinzani nchini.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here