Vituo vya afya vya kimkakati kujengwa kila jimbo

0

NAIBU Waziri, Ofisi ya Rais, TAMISEMI Zainab Katimba amesema Serikali katika Mwaka wa Fedha 2024/25 itapeleka Shilingi Milioni 250 kwa kila Jimbo, Tanzania Bara kwaajili ya kuanza ujenzi wa vituo vya afya vya kimkakati.

Katimba alisema hayo bungeni jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Moshi Vijijini (CCM) Prof. Patrick Ndakidemi aliyetaka kujua ni lini Serikali itajenga kituo cha Afya cha mkakati katika kata ya Old Moshi Mashariki.

Akijibu swali hilo, Katimba alisema Kata ya Old Moshi Mashariki ni miongoni mwa maeneo yatakayonufaika na mpango huo wa kuimarisha huduma za afya msingi.

Awali, katika swali la msingi, Mbunge wa Singida Mashariki (CCM), Miraji Mtaturu amehoji lini Serikali itatenga fedha za kujenga vituo vya afya Kata za Misughaa, Issuna na Mang’onyi.

Akijibu swali hilo, Katimba alisema Serikali inatambua uwapo wa kata ambazo hazina vituo vya afya kote nchini, ikiwamo Kata za Issuna, Misughaa na Mang’onyi katika Jimbo la Singida Mashariki.

Aidha, alisema katika mwaka wa fedha 2021/22, Serikali ilipeleka Shilingi Bilioni moja kwa ajili ya ujenzi wa Vituo vya Afya vya Ntuntu na Iglanson katika Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi na kwa mwaka 2025/26, kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri ya Ikungi itatenga Shilingi Milioni 100 ili kuendelea na ujenzi wa kituo cha afya cha Kata ya Issuna.

Alisema, Kata za Misughaa na Mang’onyi zitajengewa vituo vya afya kwa awamu kwa kuzingatia mahitaji na vigezo vilivyoainishwa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here