Viongozi wa Chadema Mwanza wadaiwa kuuza kiwanja kilichotolewa na mbunge

0

Na Mwandishi Wetu

KUMEZUKA mgogoro mkubwa kati ya viongozi na wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mkoani Mwanza, baada ya kubainika kwamba, kiwanja kilichotolewa kwa ajili ya ujenzi wa ofisi ya chama hicho kimeuzwa kinyemela.

Kiwanja hicho kilichopo Mtaa wa Ndofe, Kata ya Igoma, Wilayani Nyamagana, kilitolewa mwaka 2017 na aliyekuwa mbunge wa Viti Maalum Susan Masele na kukabidhiwa kwa Katibu wa Mkoa wakati huo Nundi Leonard, ambapo kwa mujibu wa vyanzo vyetu kutoka ofisi ya Serikali ya Mtaa huo, imethibitika kimeuzwa.

Kwa mujibu wa chanzo chetu kilichopo ndani ya Chadema kinasema, sakata la kiwanja hicho, liliibuliwa na mmoja wa wanachama ambaye alitaka kujua ukweli wa tetesi za kuuzwa kwa viwanja hicho ambacho kilipangwa kujenga ofisi ya Mkoa.

Hali hiyo, ilizua mvurugano mkubwa, ambapo wanachama waliowataka viongozi wao kutoa majibu, ingawa walishindwa kufanya hivyo na ikatafsiriwa ni njia ya kulindana.

“Wanachama walihoji kuhusu ukimya wa kiwanja kile, kulikuwa na hoja imetolewa na mwanachama mmoja ambaye aliweka wazi kwamba ana taarifa za uhakika kwamba kiwanja hicho kimeuzwa na baadhi ya viongozi,” kilisema chanzo chetu ambacho kiliomba jina lake lisitoke hadharani.

Kilisema, katika mwendelezo wa kulindana huko, mwanachama huyo aliyehoji suala hilo, alitolewa kwenye kundi ambalo lilikuwa linaendelea mjadala huo, jambo ambalo lilikoleza hasira za wanachama na kujiuliza maswali mengi.

Chanzo hicho kilisema, hasira za wanachama wengi zilitokana na kuhofia chama hicho kuingia kwenye kashfa iwapo suala hilo litatoka nje ya kundi hilo linalobeba wanachama wa mikoa ya Kanda ya Ziwa na kuhusisha viongozi wakubwa wa Kitaifa, ikizingatiwa chama hicho kwa muda mrefu kimekuwa kikijipambanua kukemea ufisadi na kutetea rasilimali za nchi.

“Wanachama walikuja juu, wakafika hatua ya kuwataka viongozi wajiuzulu kwasababu ni kashfa hiyo kubwa, wamehoji kama wenyewe tumeshindwa kusimamia rasilimali zetu, tutaweza kusimamia rasilimali za nchi siku tukikabidhiwa dola?” kilisema, akiwanukuu wanachama wenzake.

Mmoja wa wanachama ambaye alichangia mjadala huo, ambapo mwandishi wa habari hizi alionyeshwa mchango huo, aliwashutumu viongozi kwa kuhusika kwa kiasi kikubwa kusababisha kiwanja hicho kuuzwa, kwani walipaswa kuwa na utaratibu wa kukifuatilia mara kwa mara.

Walisema, waliohusika kukiuza walijua hakuna anayefuatilia kiwanja hicho ndio maana wakatumia nafasi hiyo kukiuza, ingawa iliwahi kutolewa wazo la kujenga ofisi ili kuepuka chama kufanya shughuli zake kwenye nyumba za kupanga.

“Watu wa kuwajibishwa wa kwanza ni viongozi wa Mkoa…tunahitaji safisafisha ya wazembe ianze…tujifunze kuwajibika mbele ya umma na chama. Stori ya kiwanja hiki imetuvua nguo kama chama, na watu watatumia udhaifu huu kutumaliza, ipo siku tutajikuta tupo weupe hatuna cha kujivunia,” aliandika mmoja wa wanachama. Tutavurugana sana, haya mambo tumekuwa tukiyapigia kelele CCM kumbe hata sisi huku yamejaa?” aliandika mwanachama huyo.

Mwanachama mwingine aliandika “Mimi nilishawahi kuuliza hili la kuuzwa kwa kiwanja watu wakanishambulia, na taarifa nilizipata kwa dalali wa viwanja.”

Mwanacham mwingine, alishauri kwamba wanachama hao wachange kiasi cha fedha takribani Shilingi 200,000, kisha wapeleke mawe na vifaa vingine ili waanze ujenzi kwenye eneo hilo, na hiyo itamuibua mnunuzi, akijitokeza watamuuliza aliyemuuzia kiwanja hicho na hapo watapata pakuanzia.

“Tukianza kufuata utaratibu kuanzia nyuma tutachelewa, tutakuta kiwanja kimeendelezwa, mimi nashaauri tuibue huu mgogoro ili tujue unaanzia wapi na unaishia wapi, tuweke mkeka, tuchange hela, tuweke tripu ya mawe, tukianza tripu moja, mnunuzi atajitokeza, atatuambia nani amemuuzia, atakuja na barua za mauziano tutaona nani ameuza,” alishauri mwanachama huyo.

Wengi waliunga mkono ushauri huo, ingawa walipendekeza kwamba, atafutwe Nundi ili aulizwe kuhusu suala hilo, “ushauri mzuri, lakini pakuanzia ni kwa huyo Nundi, alete hiyo mikataba ya mauziano, akigoma apelekwe mahakamani kwa kukalia mali za chama.”

Hata hivyo, pamoja na mjadala mrefu ulioendelea, ulitolewa ushauri wa kusubiri suala hilo lifanyiwe kazi baada ya Uchaguzi Mkuu, Oktoba 29, 2025, huku mmoja wa wanachama akiandika: “mimi nashauri ishu ya kiwanja ‘tu deal’ nayo baada ya tarehe 29 Oktoba, tutakuwa na nguvu na tutaweza kukichukua kwa masaa mawili tu, kikarudi mikono salama ya chama. Sasahivi naomba tuwe wapole kwanza.”

Mwandishi wa habari hizi aliwatafuta viongozi wa Chadema Mwanza waliopo sasa na waliokuwepo wakati kiwanja hicho kinakabidhiwa, lakini hawakupatikana kwa simu zao za mkononi na aliporudi kwa chanzo cha habari, alijibiwa kwamba viongozi wamepatwa na kigugumizi baada ya kuibuliwa kwa suala hilo.

“Ile ishu imewavuruga sana, hata ukiwapata hawawezi kusema chochote, wamekuwa wakikwepa kujibu kuhusu kiwanja hiki kwa muda mrefu ndio maana wanachama wameamua kuja juu, nakushauri endelea kuwabana, huku ndani wanachama wamekinukisha hasa, hali sio shwari kabisa, wanachama wanataka kujua hatma ya kiwanja hicho,” kilisema chanzo chetu ndani ya Chadema Mkoani Mwanza.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here