JOHANNESBURG, Afrika Kusini
VIONGOZI wa Afrika Kusini wameikosoa serikali ya Marekani kwa kutoa tahadhari ya uwezekano wa kutokea shambulizi la kigaidi katika nchi hiyo ya kusini mwa Afrika.
Mwishoni mwa wiki, Idara ya Taifa ya Operesheni za Pamoja na Intelijensia ya Afrika Kusini (Natjoints) iliwaonya wananchi wa nchi hiyo kuacha kusambaza taarifa za uwongo za kutokea mashambulizi ya kigaidi.
Luteni Kanali Robert Netshiunda, Msemaji wa idara hiyo inayojumuisha Idara ya Usalama wa Taifa (SSA) na Jeshi la Polisi la Afrika Kusini (SAPS) imepuuza tahadhari hiyo ya Marekani na kusisitiza kuwa, vyombo vya usalama nchini humo vimeweka mikakati ya kutosha ya kukabiliana na vitisho kwa usalama wa Taifa.
Siku ya Alhamisi, Rais Cyril Ramaphosa alikosoa tahadhari hiyo ya Marekani na kusema, “Inasikitisha kuona ubalozi wa Marekani unatoa tahadhari ya uwezekano wa kutokea hujuma ya kigaidi wikendi hapa nchini pasi na kuishauri au kufanya mazungumzo yoyote nasi.”
Ramaphosa alisisitiza kuwa: Tahadhari yoyote inapaswa kutolewa na serikali ya Afrika Kusini, lakini kwa bahati mbaya serikali nyingine imetoa tahadhari hiyo ili kuibua hofu miongoni mwa watu wetu.
Naye Zizi Kodwa, Waziri wa Usalama wa Ndani wa Afrika Kusini amesema wizara hiyo imebughudhiwa na hatua ya Ubalozi wa Marekani kutoa indhari bila kuwasiliana nayo na kuwasilisha ushahidi wa kuyapa nguvu madai yake.
Siku ya Jumatano Oktoba 26, 2022 ubalozi wa Marekani nchini Afrika Kusini ulitoa tahadhari hiyo na kudai kuwa, huenda shambulio la kigaidi likatokea Jumamosi katika eneo la Sandton, lililopo jiji la Johannesburg.