Uzinduzi wa sera ya ubia ya NHC wapata mwitikio mkubwa

0

Na Mwandishi Wetu

MENEJA Habari na Uhusiano wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Muungano Saguya, amesema baada ya kuanza kuutangazia Umma juu ya tukio la Sera ubia linalotarajia kufanyika Novemba 16, 2022 kumekuwa na mwitikio mkubwa wa makampuni binafsi ya ndani na nje ya nchi wa kushiriki uzinduzi huo.

Akizungumza na waandishi wa habari, kwenye Ofisi za Shirika hilo Jijini Dar es Salaam, Saguya alisema uzinduzi huo ambao utafanyika kwenye ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) unatarajia kukutanisha wadau takribani 1000 kutoka katika Taasisi mbalimbali za Serikali na Binafsi, vyama na Bodi za Kitaaluma, pamoja na wawekezaji binafsi wa ndani na nje ya nchi ambao tayari wamethibitisha kushiriki.

Alisema, katika uzinduzi huo pia zaidi ya Balozi 20 na Taasisi za Kimataifa 10 zitashiriki, Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Wenyeviti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), na Kamati ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma (PIC), Mawaziri, Mhimili wa Mahakama na Taasisi za Fedha.

“Kumekuwa na utayari mkubwa wa Makampuni na taasisi binafsi za nje na ndani ya nchi kutaka kuwekeza katika ujenzi wa majengo makubwa kwenye viwanja vya NHC. Kutokana na hali hiyo, Shirika limeona ni vema kuchambua na kuainisha zaidi maeneo ya kutosha ya kukidhi shauku hiyo ya kujenga nchi yetu, hapo awali tulitenga maeneo 60 tu yenye viwanja/majengo yanayohitaji kuendelezwa. Kwa msukumo uliopo sasa, tumeamua kuongeza maeneo zaidi ili yaendelezwe,” alisema Saguya.

Alisema, Shirika hilo linatayarisha vitabu viwili vitakavyoelezea sera ya ubia na maeneo ya uwekezaji ya NHC yaliyopo, yakielezea taarifa zote muhimu kwa kina.

“Kuzinduliwa kwa sera ya ubia kunaenda kufungua milango ya uwekezaji kwenye sekta ya nyumba na kwamba Shirika linaunga maono na maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ya kuvutia wawekezaji nchini kwa kuruhusu sekta binafsi ambayo ni injini ya kuleta na kujenga uchumi wa Taifa letu,” alisema Saguya.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here