Na Albert Kawogo
SALAMU zao, hakika hizi ni salamu. Hii ndio kauli inayoakisi uzinduzi mkubwa wa kihistoria wa kampeni za Chama cha Mapinduzi (CCM) ambazo kwa mara ya kwanza zimefanyika katika viwanja vya Tanganyika Packers, Kawe, jijini Dar es Salaam.
Sera nzuri za maendeleo chanya ya uchumi wa Tanzania zinazolenga kuendeleza mafanikio ya miaka mitano iliyopita, zilitawala huku mgombea urais wa CCM Dkt. Samia Suluhu Hassan akiainisha vipaumbele lukuki ambavyo ni wazi vitazidi kuipaisha Tanzania kiuchumi na kijamii.

Kampeni hizo zilipambwa na hotuba mbalimbali za viongozi wake pamoja burudani za Wasanii wa kizazi kipya taarabu, kwaya na chopa angani zilizobeba bendera za CCM.
Akiongea katika uzinduzi huo mgombea wa CCM Dkt. Samia Suluhu Hassan alijinasibu kwa kazi ambazo zilitekelezwa kwa mafanikio na Serikali katika miaka mitano ya utekelezaji wa ilani ya CCM 2020-2025.

Dkt. Samia alifafanua kuwa, Serikali imefikia malengo ya utekelezaji wa miradi ya kimkakati ikiwemo ya Miundombinu na huduma za jamii kwa mafanikio makubwa.
Mgombea huyo amesema, hawezi kusema kuwa Serikali imefanya kila kitu kwa mafanikio, lakini ameweka wazi kuwa, jitihada kubwa imefanyika ikiwemo kuifanya nchi kuwa na amani na utulivu.

“Siwezi kusema kwamba tumefanya kila kitu kilichoelezwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi, lakini kwa ujasiri mkubwa naweza kusema tumefanya makubwa kuhakikisha nchi yetu inajengwa na Taifa linarejea kwenye hali ya utulivu tuliyoizoea.” amesema Dkt. Samia.
Aidha, Dkt. Samia ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa CCM ametaja mambo atakayoanza nayo siku 100 za kwanza kipindi cha pili cha uongozi wa Awamu ya Sita.

Amesema, katika utekelezaji wa sheria ya Bima ya afya kwa wote, Serikali ya CCM itazindua rasmi mfumo wa Taifa wa bima ya afya kwa wote ikianzia watoto na watu wenye ulemavu, ambapo gharama zitabebwa na Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF).
Pia, Dkt. Samia amesema itapiga marufuku hospitali yoyote nchini kuzuia ndugu kuchukua mili ya marehemu pale gharama za matibabu zinapokuwa hazijalipwa akiahidi kuanzisha utaratibu mpya wa kushughulikia changamoto hiyo.

Awali, akiongea kwenye uzinduzi Rais Mstaafu wa awamu ya nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alisema, tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi, Chama cha Mapinduzi kimekuwa na utamaduni wa kutokuwashindanisha ndani ya chama wagombea wake wa Urais pindi wanapoomba kugombea kipindi cha pili.
“Tumekuwa na utamaduni huo wa kuwapa nafasi ya kugombea kipindi cha pili bila upinzani,imefanyika hivyo kwa Mzee Mkapa, ikafanyika hivyo kwangu na baadae kwa Dkt. Magufuli sasa iweje nongwa kwa Dkt. Samia?” Alisema Dk Kikwete.

Dkt. Kikwete alifafanua kuwa, wanaohoji uhalali wa Dkt. Samia kupitishwa bila kupingwa, huenda hawajui historia ya CCM na pengine hawakijui Chama cha Mapinduzi kabisa.
Pazia la kampeni kwa CCM ndio limezinduliwa rasmi sasa ambapo mgombea wake Dkt. Samia Suluhu Hassan atazunguka nchi nzima kuinadi ilani ya Chama cha Mapinduzi ya 2025/2030 huku akiomba ridhaa ya watanzania kuipa nafasi tena CCM ili iweze kuongoza dola.
