Na Mwandishi Wetu
MKURUGENZI Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) Dkt. Aneth Komba amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi kutoka Programu ya Shule Bora kujadili namna bora ya kuendelea kushirikiana katika kutekeleza Mtaala ulioboreshwa ambao tayari umeanza kutekelezwa.
Kikao hicho kilihudhuriwa na baadhi ya wajumbe wa menejimenti na wakuza Mitaala kimefanyika leo Januari 23, 2024 katika ofisi za TET Jijini Dar es Salaam ambapo lengo ni kujadili namna bora ya kuboresha utoaji elimu nchini hasa katika eneo la Mitaala.
Dkt. Komba alisema, katika utekelezaji wa Mitaala hiyo kipaumbele cha Serikali kupitia Taasisi ya Elimu Tanzania ni kutoa mafunzo kwa walimu ili kuwajengea uwezo kuhusu namna bora ya kuendelea kutekeleza Mtaala ulioboreshwa kwa kiwango kinachotakiwa.
Aliendelea kusema, Taasisi ya Elimu Tanzania inashukuru ushirikiano uliopo na inatambua mchango unatolewa na mradi wa Shule Bora, hasa katika kipindi hiki ambacho Serikali inaendelea kutekeleza Mtaala ulioboreshwa.
Aidha, Dkt. Komba alisema, Taasisi inaendelea kutekeleza mfumo wa mtandao wa kujifunzia (Learning Management Systems) unaotoa fursa kwa walimu kujifunza zaidi kuhusu Mitaala na ujuzi mwingine, huku akisisitiza mfumo huu utasaidia kupunguza gharama ya utoaji mafunzo na kuongeza idadi kubwa kwa walimu waliopata mafunzo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa mafunzo ya Mitaala Dkt. Fika Mwakabungu alisema, kupitia programu ya Shule Bora inayotekelezwa katika mikoa tisa, idadi ya walimu waliopata mafunzo kuhusu Mtaala ulioboreshwa imeongezeka hasa walimu wa somo la Kiingereza.
Alisema, licha ya Taasisi kwa kushirikiana na wadau kuendelea kutoa mafunzo kwa walimu, Taasisi inaendelea kusisitiza utekelezaji wa mpango wa MEWAKA unaotoa fursa kwa walimu kujifunza katika maeneo ya kazi ili kuongeza ujuzi zaidi katika Mitaala na ujuzi mwingine.
Naye, Mkurugenzi wa machapisho kutoka Taasisi ya Elimu Tanzania Kwangu Kwangu alisema, Taasisi inaendelea kuwashawishi walimu kuendelea kutumia mfumo wa (Learning Management System) ambao unatoa fursa ya kujifunza mahali popote bila gharama kubwa na muda mfupi.