Ushindani wa demokrasia si kuachiana madaraka kiushemeji – Mbeto

0

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema siku moja ikitokea kimeshindwa Uchaguzi kwa matakwa ya demokrasia, hakitasita kukubali matokeo, lakini hakitakiachia chama chochote utawala kwa huruma, ushemeji na hisani.

CCM kimesistiza, upinzani wa Zanzibar haujapevuka na kuwa madhubuti kiasi cha kuwaridhisha wananchi ushike madaraka.

Hayo yameelezwa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC za Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamisi Mbeto Khamis wakati akimjibu Mgombea Urais wa ACT Wazalendo Othman Masoud Othman.

Mbeto alimueleza Othman kuwa, wananchi bado hawakijakiamini ACT Wazalendo aidha kwa itikadi na sera zake, misimamo yake na aina ya viongozi walionao ili kipigiwe kura za kushika utawala.

Alisema, Wananchi hususan wa Zanzibar ni wakomavu kisiasa, werevu, wanaopima mambo bila kukurupuka, hivyo hawajapata sababu ya kukiacha CCM na kuuchagua upinzani.

“Upinzani bado una kazi ya kujitafakari. Lazima wajue kwanini wananchi wanawakataa. Matamshi yao hayaonyeshi kujali umoja, viongozi wake wamejawa ubaguzi huku wengi wao wakihusishwa na tabia chafu za uhuni,” alisema Mbeto.

Aidha, Katibu huyo Mwenezi alisema, kujenga Taasisi ya kisiasa imara inayoaminiwa na wananchi, si jambo la muda mfupi, badala yake ni mchakato unaohitaji kupata sera mbadala, hoja yakinifu na dira sahihi.

“ASP toka mwaka 1957 kimevibwaga vyama vya ZNP na ZPPP. Vyama hivyo havikutokana na matakwa ya wengi. Wananchi wote waliunga mkono Sera za ASP na wagombea wake,” alikumbusha.

Mbeto alisema, kizazi cha sasa kuelekea miaka hamsini ijayo, ni kile kilichotokana na Mapinduzi
ya Zanzibar mwaka 1964 ambayo ndiyo yaliyovunja matabaka na utawala uliodumu miaka 104.

“Makundi ya wananchi wa kizazi hiki wamesomeshwa kwa sera za CCM. CCM kimerithi sera za TANU na ASP. SMZ imekomesha ubaguzi, upendeleo na inawajali wanyonge na masikini,” alieleza.

Alisema, wanapotokea Wanasiasa wa upinzani na kuanza kuhubiri sera zisizoijengea matumaini jamii na kuhubiri chuki, ubaguzi na ukabila, wananchi wana haki ya kuvikataa vyama hivyo.

“Mgombea anaposema utatoa nchi taka usitake huyo ameshabaini atashindwa. Anapotumia lugha ya vitisho na kudhani atashika madaraka kwa ushemeji na ukwe, asahau jambo hilo,” alisisitiza Mbeto.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here