Na Fatma Jalala
KUNA msemo wa kale usemao, “Mtu wa kweli huonekana katika dhoruba, si kwenye upepo wa utulivu.” Ndivyo ilivyo katika dunia ya uongozi, kila kiongozi makini hupitia upepo wa maneno, dhoruba za upinzani, na majaribu ya kutoeleweka.
Ni kipimo cha uthabiti, si udhaifu. Kiongozi wa kweli hujengwa na changamoto, huimarishwa na mashambulizi ya maneno, na hupewa nguvu na imani ya wale wanaoona mbali kuliko kelele za muda.
Dkt. Samia Suluhu Hassan ni mfano hai wa hekima hiyo. Amepitia dhoruba za upotoshaji, kejeli na mashaka, lakini amebaki imara, akiongoza kwa utulivu unaotisha wenye hila na unyenyekevu unaovutia wenye busara. Ujasiri wake si wa makelele bali wa matokeo.
Amechagua kuongoza kwa hekima badala ya jazba, kusikiliza badala ya kulipiza, na kujenga badala ya kubomoa. Ni kiongozi aliyechagua kutembea njia ya mawe, si ya maua, akijua kuwa urithi wa kweli hauandikwi kwa maneno matamu, bali kwa alama zinazobaki vizazi baadae.
Katika kila enzi, historia imekuwa na namna yake ya kuwatenga wanyonge wa fikra na kuwatukuza wenye maono. Wapo leo wanaomkosoa Dkt. Samia kwa maneno yasiyo na mizani, lakini kesho historia itawakumbuka kama mashuhuda waliokuwa macho lakini hawakuona.
Watasimulia yale waliyojaribu kuyapinga. Kama methali isemayo, “Mhemea nyumba ya ufa ndiye mpazi,” wale wanaoikosoa leo Serikali yake, watakuwa wa kwanza kunufaika na kazi zake. Ni ukinzani wa maisha kwamba ukosoaji wa leo ndio ushuhuda wa kesho.
Ukweli ni huu usiofutika: Tanzania ipo katika njia sahihi. Sauti za shaka haziwezi kuzima nuru ya maendeleo, wala kelele za upotoshaji haziwezi kufunika sauti ya ukweli. Dkt. Samia ameonyesha dunia kuwa uongozi wa mwanamke hauhitaji mabavu bali busara; hauhitaji makelele bali matokeo; hauhitaji nguvu ya misuli bali nguvu ya fikra.
Nilijifunza haya kwa macho yangu. Nikiwa kiongozi wa taasisi fulani, nilipitia changamoto nyingi, maneno makali, hila, na mashaka kutoka kwa wale niliowaongoza. Ilifika mahali moyo ulitaka kulegea, nguvu zikaanza kupungua. Lakini, kila nilipomtazama Dkt. Samia, nilipata nguvu mpya. Nilimwona kama dira ya uongozi wa kweli, ‘role model’ wa uthabiti.
Nilijiambia kimoyomoyo, “Mimi nawajibika kwa watu wachache tu katika mkoa mmoja, tena waliochagua kuwa sehemu ya taasisi hii. Vipi kuhusu Mama huyu anayewatumikia Watanzania milioni zaidi ya sitini? Changamoto anazopitia yeye ni kubwa mara mia, lakini bado anasonga mbele bila kuyumba.”
Nilijifunza kuwa uongozi ni tendo la moyo, si la heshima. Ni sadaka ya utu, si biashara ya sifa. Nilipoona namna Dkt. Samia anavyotulia mbele na kuiendesha nchi bila kuyumba, nikatambua kwamba nguvu ya kweli haiko kwenye kukemea bali kuvumilia. Akili ya kiongozi haionekani anaposhangiliwa, bali anapovumilia lawama na bado akaendelea kutenda mema.
Mbali na changamoto nilizopitia, nimejifunza kuwa na hasira yenye maadili, hasira ya kuona taifa langu likipiga hatua, si hasira ya kuonesha ubabe, sababu yupo Mama anayetuonesha njia, Mama anayepanda mbegu ya matumaini katika udongo uliojaa mawe ya maneno ya kifedhuli.
Kila ninapomtazama, najikumbusha kuwa kiongozi si lazima apendwe, bali aheshimiwe kwa kazi zake.
Uongozi wa Dkt. Samia ni somo la kifalsafa kuhusu maana halisi ya nguvu tulivu. Amefanikisha mageuzi ya kiuchumi, kijamii na kidiplomasia bila fujo, bila jazba, na bila majivuno. Ameweka mizani ya uongozi unaojali utu kuliko maneno, na kazi zake zinajibu maswali ya wanaodai maelezo.
Kwa macho ya wengi, yeye ni Mama wa taifa si kwa jina, bali kwa matendo. Amejenga miundombinu, ameimarisha diplomasia, amefungua fursa kwa wanawake na vijana, na kurejesha imani kwa Watanzania kuwa taifa letu lina mwelekeo. Yote haya yanaonyesha kuwa busara ni nguvu, na uongozi wa kweli hauhitaji kutangaza bali unajitangaza kwa matokeo.
Tunao wajibu wa kutembea kifua mbele, si kwa majivuno, bali kwa fahari ya kuwa sehemu ya zama za mageuzi haya. Tumuunge mkono, tumlinde, tumsemee, maana historia haimsubirii mtu. Wale wanaojaribu kuchafua ukweli leo watabaki kuusimulia kesho kwa aibu.
Hivyo, tusiruhusu ukweli huu usiofutika utusababishie kuja kutahayari baadaye. Tujifunze kutambua thamani ya kiongozi wetu wakati bado yupo kazini. Tukome kutumia akili za maneno, tujenge akili ya matendo. Kwa sababu uongozi wa kweli kama ule wa Dkt. Samia hauna hofu ya kupingwa, bali hofu ya kusaliti maono, haki na utu.
Na katika haya, tunayo kila sababu ya kuitumia haki yetu ya Kikatiba kwa kwenda kupiga kura tarehe 29 Oktoba mwaka huu siku chache tu zilizobaki kumchagua kiongozi mahiri anayestahili kutuongoza kwa misingi ya uwezo na utendaji aliouonesha katika kipindi kilichopita.
Tuweke akilini kuwa historia huandikwa kwa kalamu isiyofutika; na katika kurasa zake, jina la Dkt. Samia Suluhu Hassan litabaki limechorwa kwa wino wa hekima, ujasiri na uthubutu wa kweli.