‘Ujenzi Bwawa la kufua umeme la Julius Nyerere unaridhisha’

0

Na Neema Mbuja, JNHPP

KAMATI ya kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeridhishwa na kasi ya ujenzi wa mradi wa bwawa la kufua umeme la Julius Nyerere unaotekelezwa na mkandarasi kutoka Misri wa kampuni ya ELSEWEDY na kugharimu kiasi cha Shilingi Trilioni 6.5 pindi utakapokamilika na hivyo kuimarisha hali ya upatikanaji wa umeme bora na uhakika kwenye gridi ya Taifa.

Akizungumza wakati wa majumuisho baada ya kutembelea mradi huo, Kaimu mwenyekiti wa kamati hiyo ya kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Mhandisi Stella Manyanya alisema, kamati imeridhishwa na hatua za ujenzi kufikia asilimia 74 ikilinganishwa na asilimia 67 zilizopita na kulipongeza Shirika la umeme Tanzania TANESCO kwa kusimamia vema mradi huo na kumekuwepo na mabadiliko ya wazi yanayoonekana kila wakati

Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi Mtendaji-Usambazaji Mhandisi Athanasius Nangali amesema kuwa kwa sasa vifaa kwa ajili ya ujenzi wa mradi vimeshawasili ikiwemo TRANSFOMA 29 za njia moja zenye ukubwa wa 92.2 MVA ambazo zitatumika kwenye kituo cha kupoza umeme kutoka kampuni ya ABB.

Kamati ya Bunge ya kudumu ya Nishati na Madini ilitembelea eneo linakojengwa tuta kuu la kuhifadhi maji yaani ‘main Dam’ ambalo lina sehemu kuu tatu yaani upande wa kushoto, kulia na kati na urefu wa mita 1025 na kimo cha mita 190 kutoka usawa wa bahari.

Eneo lingine walilotembelea ni jengo la mitambo yaani Power House ambapo itasimikwa mitambo 9 yenye uwezo wa kufua umeme wa Megawati 235 kwa kila moja, pia walifanikiwa kuona hatua zinazoendelea eneo zilikosimikwa mashine Umba yaani Transfoma ambazo zitatumika kwenye kituo cha kupooza umeme kabla ya kusafirishwa kuingia kwenye gridi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here