Uandikishaji daftari la wapiga kura kuanza Wilaya wa Kusini, Unguja

0

Mwandishi Wetu, Zanzibar

DAFTARI Daftari la Kudumu la Wapiga kura Zanzibar linahitimishwa leo Machi 10, 2025 Wilaya ya Kati na kesho linaanza Wilaya ya Kusini, Unguja.

Akizungumza na Afrika Leo, Katibu wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis alisema daftari hilo linaingia mkoa huo baada ya kutamatika katika Mkoa wa Mjini Magharibi.

Mwenezi Mbeto alisema, kulingana na ratiba ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), daftari limeanzia Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini, Machi 8, 2025 na uandikishaji unaendelea vizuri.

Alibainisha kuwa, zoezi la uandikishaji wa daftari hilo lililoanzia Visiwani Pemba, litafungwa Machi 15, 2025 Wilaya ya Mjini na amehimiza wananchi kujitokeza kujiandikisha.

Daftari hilo ambalo linaandikisha wapiga kura wapya wenye sifa na wengine kurekebisha taarifa zao ni sehemu ya safari ya kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025.

Kulingana na ZEC wanaostahili kuandikishwa ni wote wenye sifa ya ukaazi wa Zanzibar.

Sheria Namba 4 ya Mwaka 2018 imetaja wenye sifa ya kuandikishwa ni Mzanzibari yeyote, aliyetimiza miaka 18 mwenye kitambulisho cha Ukaazi aliyeishi kwenye jimbo na Shehia miezi thelathini na sita mfululizo na ambaye jina lake lipo kwa Sheha wa Shehia anayoishi.

Pia, sheria inamtaja Mtanzania yeyote aliyeishi Zanzibar zaidi ya miaka 10 mwenye kitambulisho cha Ukaazi na jina lake lipo kwenye kumbukumbu za Sheha, ataandikishwa kuwa mpiga kura.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here