Tuwalee vijana katika maadili na tudumishe amani – Rais Mwinyi

0

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ametoa wito kwa wazazi, walezi, jamii na waumini wa dini ya Kiislamu kwa ujumla kuwalea vijana katika maadili mema, huku akisisitiza umuhimu wa kudumisha amani hasa tunapoelekea katika kipindi cha uchaguzi.

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo Julai 11, 2025, mara baada ya kusali Sala ya Ijumaa, Masjid Lilah Kianga, Mkoa wa Mjini, Wilaya ya Magharibi ‘A’.

Katika salamu zake, Rais Dkt. Mwinyi amegusia maudhui ya Khutba ya Ijumaa iliyolenga malezi bora ya vijana na umuhimu wa kusali, akibainisha kuwa vijana wengi wamekuwa wakikosa mwelekeo sahihi na kujiingiza katika vitendo viovu kama vile dawa za kulevya, ujambazi na wizi, hali inayosababisha mmomonyoko wa maadili katika jamii.

Halikadhalika, Rais Dkt. Mwinyi ameshukuru uongozi wa msikiti wa Masjid Lilah kwa kumpa fursa ya kutoa salamu, akisisitiza kuwa viongozi wa dini wana nafasi muhimu katika kulea jamii kimaadili na kiroho.

Rais Dkt.Mwinyi ameeleza kuwa maendeleo, ibada na ustawi wa jamii haviwezi kupatikana bila kuwepo kwa amani ya kudumu. Kwa msingi huo, amehimiza viongozi wa dini na wa kisiasa kushirikiana kuhakikisha amani inaendelea kulindwa na kuenziwa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here