‘Tutumie fursa kukuza lugha ya kiswahili kwenye CHAN’

0

KAIMU Mkurugenzi wa Idara ya Habari-MAELEZO Rodney Thadeus amesema miongoni mwa fursa ambazo Tanzania itapata kwenye mashindano ya kuwania Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ligi za Ndani (CHAN 2024) ni pamoja na kuitangaza lugha ya Kiswahili kwa wageni watakaokuja kwa ajili ya michuano hiyo.

Ameyasema hayo Julai 26, 2025 katika mahojiano na Kipindi cha Besera cha TBC Redio Jamii Dodoma alipokuwa akizungumzia fursa zitakazojitokeza kwenye michuano ya CHAN 2024 ambayo inatarajia kuanza Agosti 2, 2025 kwenye nchi za Tanzania, Kenya na Uganda.

“Hii ni fursa nyingine kwa nchi na kwa lugha yetu ambayo inazidi kusambaa kwa kasi, unapotumia lugha ya kiswahili kwenye michuano hiyo maana yake hata mataifa mengine yatatoka na kutazaliwa maneno ambayo wataondoka nayo wageni, na wakipata maneno mawili matatu ya kiswahili huwa wanakumbuka kuwa haya maneno niliyapata Tanzania” alisema Rodney.

Alisema, wageni wanapokuja kwenye michuano hiyo pia watapata huduma mbalimbali za kijamii kutoka kwa wananchi ambao wanazungumza lugha ya kiswahili, hivyo Tanzania ina nafasi kubwa ya kutangaza lugha yake yenyewe.

“Unajua kiswahili hakitumiki uwanjani tu, mashindano yanapokuja yanakuja na fursa zingine, kwa hiyo wachezaji na mashabiki wanapokuja nao watapata huduma mbalimbali kama hotelini, madukani, kumbi za muziki, hivyo lugha yetu itazidi kukua,” alisema Rodney.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here