THE CIVIC UNITED FRONT (CUF- Chama Cha Wananchi)
SALAMU ZA RAMBIRAMBI KUFUATIA KIFO CHA RAIS MSTAAFU MHESHIMIWA ALI HASSAN MWINYI:
CUF- Chama Cha Wananchi kimepokea kwa simanzi, huzuni na masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili ya Uongozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Ali Hassan Mwinyi kilichotokea jioni ya leo.
Watanzania tumeondokewa na ‘Baba wa Demokrasia’, aliyeruhusu Mfumo wa Demokrasia ya Vyama Vingi nchini mwaka 1992 akiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Marehemu Mwinyi atakumbukwa kwa Utawala Bora unaodhihirisha kuwajali na kuwahurumia Watanzania, kwa jitihada zake za kuwaondoa katika mazingira magumu sana ya kukosa bidhaa muhimu ikiwa ni pamoja na vyakula kama mchele, unga na sukari pamoja na bidhaa zingine ikiwa ni pamoja na sabuni na mavazi. Aliipokea nchi ikiwa katika hali ya umaskini wa kupitiliza na msamiati wa ‘bidhaa hadimu’ ulikuwa maarufu kwa kuwa bidhaa muhimu zilihadimika na kusababisha hali ngumu sana kimaisha. Marehemu Mwinyi aliufuta msamiati huo kwa kufanikisha kupatikana tena bidhaa zilizokuwa zimehadimika. Aidha, marehemu Ali Hassan Mwinyi ameweka historia ya kuwa Mwalimu wa Uwajibikaji pale alipoamua kujiuzulu Uwaziri kutokana na makosa yaliyofanywa na watumishi kwenye Wizara aliyokuwa akiiongoza na kusababisha maafa.
Tunamuomba Mwenyezi Mungu ampe kauli thabiti na kumuingiza kwenye Pepo ya Firdaus. CUF- Chama Cha Wananchi kinatoa pole kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na mtoto wa Marehemu Dkt Hussein Ali Mwinyi, ndugu, jamaa, marafiki na Watanzania wote kutokana na msiba huu mzito. Ni muhimu kuwa na Subira njema katika kipindi hiki cha majonzi na simanzi.
HAKIKA SISI NI WA ALLAH NA KWAKE SOTE TUNAREJEA!
HAKI SAWA KWA WOTE!
Prof. Ibrahim Lipumba
Mwenyekiti Taifa
CUF- Chama Cha Wananchi
Februari 29, 2024