KATIKA muendelezo wake wa kukutana na watu wa makundi mbalimbali kwa ajili ya kusikiliza Ushahidi wao kuhusu Matukio ya Uvunjifu wa Amani yaliyojitokeza wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, Tume ya Uchunguzi wa Matukio hayo imetembelea Gereza Kuu Arusha.
Ikiwa katika gereza hilo tume imezungumza na Watendaji Wakuu wa gereza na Mahabusu 10 waliobakizwa katika gereza hilo wakiwemo wanaume 9 na mwanamke mmoja wote wakitarajiwa kurudi Mahakamani Januari 14 mwaka huu.
Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji Mkuu Mstaafu Othuman Chande amesema tume hiyo inasikiliza na kuzungumza na watu wa makundi mbalimbali ili kubaini kiini cha matukio hayo ili yasijirudie tena.
Naye Mkuu wa Gereza hilo, Vicent Karani amesema jumla ya mahabusu waliopokelewa gerezani hapo walikuwa 197 na mahabusu 187 waliachiliwa na mahakama na mahabusu waliobaki gerezani hapo ni 10 ambao wameongezewa kosa la pili.
Tume hiyo inaendelea na mahojiano na waathirika wa Matukio hayo mikoa mbalimbali ikiwemo Arusha, Mwanza na Mbeya ikiwa na lengo la kubaini kiini cha matukio hayo na kuwasilisha kwa ajili ya hatua zaidi kama Taifa ili yasijirudie tena.