TPHPA yavunja rekodi ya makusanyo

0

MAMLAKA ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) imevunja rekodi baada ya kukusanya Shilingi Bilioni 6.14 kwa kipindi cha miezi mitatu.

TPHPA ambayo ilianza kazi rasmi Julai, 2022, ikiundwa kwa Sheria ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Na.4 ya mwaka 2020 (Plant Health Act No. 04 of 2020, ilitarajia kukusanya Shilingi Bilioni 6.45 ndani ya mwaka mmoja.

Mkurugenzi Mkuu wa TPHPA Prof. Joseph Ndunguru alisema hayo jijini Dar es Salaam leo, Machi 13, 2024 wakati akizungumza na Wahariri na waandishi wa Vyombo mbalimbali vya habari kupitia utaratibu maalum unaoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR).

Prof. Ndunguru alisema, katika mwaka wa Fedha 2023/2024 Mamlaka hiyo ilikusudia kukusanya kiasi cha fedha cha Shilingi Bilioni 6,454,437,453, mapato ya ndani na katika kipindi cha kuanzia Julai 2023 hadi Septemba 2023, Mamlaka hiyo imefanikiwa kukusanya kiasi cha Shilingi 6,143,965 337.61 (95.2%) ya makadirio ya makusanyo ya mwaka mzima kutoka kwenye vyanzo vyake mbalimbali vya mapato ya ndani.

“Tunatarajia hadi kufikia mwisho wa mwaka wa fedha, Mamlaka itaweza kukusanya zaidi ya 100% ya makadirio hayo na hivyo kuweza kuongeza kiazi cha gawio lake kwa serikali kuu (15%) (Government Remitance) kutoka Shilingi  968,165,000.62 tulizotarajia hadi Shilingi 3,686,379,202.56 kwa mwaka,” alisema Prof. Ndunguru.

Aliongeza:“Kwa kipindi cha mwezi Oktoba mpaka Disemba 2023 Mamlaka imekusanya kiasi cha Shilingi 5, 352, 196, 967.04. Kwa kipindi cha Januari mpaka Machi 6, 2024 Mamlaka imekusanya kiasi cha Shilingi Bilioni 3.7.”

Akitaja baadhi ya majukumu ya Mamlaka hiyo kwenye mkutano huo, Prof. Ndunguru alisema, TPHPA iliundwa ili kusimamia na kudhibiti afya ya mimea, mazao ya mimea na viuatilifu.

Pia, wana jukumu la kudhibiti uagizaji, usafirishaji, utengenezaji, usambazaji, uuzaji, na matumizi ya viuatilifu na vifaa vya unyunyiziaji wa viuatilifu ili kuleta tija katika Kilimo.

Aidha, TPHPA inafanya ukaguzi na ufuatiliaji wa usafi wa mimea na mazao mashambani, ghalani na mipakani ili kuzuia kuenea kwa visumbufu.

“Mamlaka hii ina jukumu kubwa la kuhakikisha kuna mazingira salama kwa afya ya binadamu, wanyama na mimea kwa kuwa na matumizi sahihi na salama ya viuatilifu nchini,” alisema.

Alisema, kama yalivyo Mashirika mengine ya umma ambayo yapo chini ya Ofisi ya Msajili Hazina, nao wanatekeleza maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha wanafanyia mageuzi mashirika hayo ili kuongeza tija kwa Taifa.

“Tumedhamiria kuwa chombo mahiri kinachoongoza katika kutoa huduma za afya ya mimea katika udhibiti wa visumbufu vya mimea na viuatilifu kwa kiwango cha Kimataifa,” alisema Prof. Ndunguru.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here