TPA yanadi fursa za uwekezaji katika bandari zake

0

MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imetumia fursa ya maonesho ya Tamasha la Biashara na Utalii Kusini kunadi fursa za uwekezaji katika bandari zake hapa nchini.

Maonesho hayo, yaliyofunguliwa rasmi na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Mabunge ya Jumuiya ya Madola, Dkt. Tulia Ackson, linafanyika katika viwanja vya fukwe za Ziwa Nyasa, eneo la Matema Beach, Wilayani Kyela, jijini Mbeya.

Akizungumza wakati wa maonesho hayo, Afisa Uhusiano Mwandamizi wa TPA, Leonard Magomba, alisema, kwa TPA, maonesho hayo ni fursa muhimu ya kunadi maeneo mbalimbali ya uwekezaji katika bandari zetu pamoja na kuelezea wadau maboressho mbalimbali ya miundombinu yanayoendelea na yaliyokwisha fanyika.

“Sote ni mashahidi wa faida za ushirikiano kati ya TPA na wawekezaji katika bandari zetu. Ufanisi umeongezeka sana hususan katika Bandari ya Dar es Salaam ambapo tunashirikiana vyema na wabia wetu, ambao ni Kampuni za DP World na Tanzania East Africa Gateway Terminal Ltd,” alisema.

Tangu kuanza kazi kwa wabia, ufanisi katika Bandari ya Dar es Salaam umeongezeka kwa kiwango kikubwa, hali iliyowezesha kuvuka lengo la kuhudumia shehena ya tani Milioni 27 kabla ya muda uliotarajiwa kufikia mwaka 2028. TPA iliweka lengo la kuhudumia kiwango hicho cha shehena ifikapo mwaka 2027, lakini miaka mitatu kabla, tayari leo hilo limefikiwa.

Mbali na mafanikio hayo, TPA imejipanga kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika bandari zake ili kufungua zaidi milango kwa wawekezaji.

Uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali kupitia TPA katika Bandari ya Dar es Salaam umetoa fursa za uwekezaji katika bandari hiyo ambapo, kwa sasa, TPA inafanya kazi kwa mafanikio makubwa na wabia wake.

Katika Bandari ya Dar es Salaam, TPA imefanya maboresho makubwa katika miundombinu, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa magati ya kisasa, kuongeza kina hadi mita 14.5, na kupanua eneo la kugeuzia meli na lango la kuingia bandarini.

TPA pia imefanya maboresho katika Bandari ya Tanga kwa kuongeza kina na kuboresha magati yake, huku Bandari ya Mtwara ikijengwa gati mpya namba 2 lenye urefu wa mita 300.

Kwa upande wa Bandari za Maziwa, Serikali kupitia TPA inaboresha miundombinu katika Bandari za Mwanza Kaskazini, Kemondo, na Bukoba kwa upande wa Ziwa Victoria. Katika Ziwa Nyasa, TPA inajenga bandari mpya na ya kisasa ya Mbambabay ambayo itakuwa na uwezo wa kuhudumia hadi makasha, huku katika Ziwa Tanganyika, TPA ikijenga bandari za kisasa za Karema, Kabwe, Ujiji, na Kibirizi.

Mbali na kuelezea fursa za uwekezaji, TPA ilipata fursa ya kunadi bandari zake kwa wadau wa ndani na nje ya nchi ili kuongeza shehena ya mizigo.

Mwaka huu 2024, Tamasha la Biashara na Utalii Kusini limehusisha taasisi za kiserikali, za umma, binafsi, na wafanyabiashara wadogo kutoka ndani na nje ya nchi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here