Na Mwandishi Wetu
MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imesema kwamba, inaendelea na kampeni kubwa ya kurasimisha bandari bubu (bandari zisizo rasmi) ili kuepuka uvujaji wa mapato na kulinda afya za watanzania.
Akizungumza kwenye Mkutano Mkuu wa 13 wa Kitaaluma wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), uliofanyika hivi karibuni, kwenye ukumbi wa St. Gaspar, Mjini Dodoma, Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Mrisho Mrisho alisema, bandari zisizo rasmi ni changamoto kubwa ambayo wanaendelea kupambana nayo.
“Ufukwe wetu ni mrefu na kwa mhalifu anayekusudia kutenda uovu anatumia hayo maeneo, ni kama kiumbe akishajua mmefika hapo anahama, anakwenda kwingine, athari za bandari zisizo rasmi ni nyingi ikiwemo uvujaji wa mapato, pia bidhaa inayopita inashindwa kuratibiwa na kama ina madhara kwa vyakula, maana yake inaathiri walaji,” alisema Mrisho.
Alisema, kwa kipindi cha miaka mitatu sasa wanaendelea na kampeni kubwa ya kuainisha maeneo ambayo yamekuwa sugu katika upitishaji wa bidhaa kwa njia za magendo ili kuyarasimisha kwa mujibu wa sheria.
“Yale maeneo ambayo yana mwonekano wa bandari kwa mfano Mbweni tumeyarasimisha, kwa maana kwamba taasisi zote za Serikali zinazohusika na bandari zipo pale,” alisema.
Hata hivyo, alisema pamoja na kampeni ambayo wanaendelea nayo, bado wanakabiliwa na uhaba wa miundombinu kwenye bandari zilizo rasimishwa, kwani bado haijakamilika.
“Changamoto iliyopo ni miundombinu haijakamilika, Kunduchi halikadhalika, kwa hiyo wahalifu hawaji, wanakwenda kuanzisha kwingine, hivi karibuni Waziri Mkuu amezindua boti itakayokuwa inafanya doria kwenye maeneo ya baharini,” alisema.
Katika kuhakikisha kampeni yao inafanikiwa, TPA wanapanga kushirikisha Mamlaka za Serikali zilizopo kwenye maeneo yanayorasimishwa “Tunakusudia kama ni halmashauri, ni kijiji tukabidhi hayo maeneo ili yawe kwenye uangalizi wao,”
“Hayo ndiyo tunayoyafanya sisi kama TPA, hatuna watu wa kuwaweka kwenye ufukwe wote, ila ni jambo linalohusisha taasisi nyingi, kwa kweli nikiri changamoto ya bandari zisizo rasmi ni nyingi na ufukwe huu ni mkubwa,” alisema Mrisho Mrisho ambaye kweye mkutano huo alimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Plasduce Mbossa.