WAZIRI wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Kairuki amesema mafunzo ya TEHAMA kwa walimu wa shule za sekondari nchini yanalenga kuwajengea walimu ujuzi wa kutumia teknolojia, ili waweze pia kuwahamasiaha wanafunzi kutumia teknolojia katika ujifunzaji.
Akizungumza jana, Januari 5, 2026, wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo yaliyofanyika katika Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Waziri Kairuki amesisitiza umuhimu wa walimu kushiriki kikamilifu mafunzo haya ili kupata ujuzi unaohitajika.

Jumla ya walimu 606 kutoka mikoa yote ya Tanzania watapatiwa mafunzo kwa muda wa siku tano katika vituo vitatu ambavyo ni; Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST), na Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT).
Aidha, Waziri amewataka walimu kuzingatia mafunzo haya na kuweka umakini mkubwa katika kujifunza, akisisitiza kwamba ujuzi wa TEHAMA ni nyenzo muhimu itakayowawezesha wanafunzi kuwa wabunifu wa teknolojia pamoja na kuwaandaa kumudu soko la ushindani wa ajira katika siku zijazo.
