TBS yafikia asilimia 99 ya lengo la ukaguzi wa shehena

0
Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt Athumani Ngenya.

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) kwa kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, limefikia asilimia 99 ya lengo la ukaguzi wa shehena zinazotoka nje ya nchi.

TBS hudhibiti ubora wa bidhaa zinazoingizwa nchini kutoka nje kwa kutumia mfumo wa ‘Pre-Shipment Verification of Conformity to Standards (PVoC)’ pamoja na kufanya ukaguzi pindi bidhaa zinapowasili nchini.

Akizungumza jijini Dar es Salaam kwenye Mkutano na Wahariri na Waandishi wa habari, ulioandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR), Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt Athumani Ngenya alisema, shehena 100,851 zilikaguliwa kabla hazijaingizwa nchini, ambapo lengo lilikuwa kukagua shehena 102,083.

“Pia, jumla ya bidhaa 151,570 kutoka nje ya nchi zilikaguliwa baada ya kufika nchini sawa na asilimia 77 ya lengo la kukagua bidhaa 197,417,” alisema Dkt. Ngenya.

Aidha, Mkurugenzi huyo alisema, mbali na mafanikio hayo ya ukaguzi wa bidhaa na shehena, pia wametoa wametoa leseni za ubora 2,106 kwa wazalishaji mbalimbali wa bidhaa hapa nchini. “ni sawa na asilimia 105.3 ya lengo la kutoa leseni 2,000, huku leseni 1,051 zilitolewa bure kwa wajasiriamali wadogowadogo.”

Dkt. Ngenya alisema, wajasiliamali waliopewa leseni hizo 1,051 bidhaa zao zimethibitishwa na zinauzwa ndani na nje ya nchi. “Pia, tumetoa mafunzo kwa wadau 5,786 kutoka mikoa mbalimbali”

Katika hatua nyingine, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Dkt. Athumani Ngenya (TBS) alisema kwa kipindi cha miaka mitatu, wamefanikiwa kutoa gawio kwa Serikali Shilingi Bilioni 18.1.

Alisema, wametoa gawio hilo ili kutoa mchango wao katika miradi mikubwa ya kimkakati inayotekelezwa nchini na inayohitaji fedha nyingi ukiwemo mradi wa Treni ya Kisasa (SGR), Bomba la Mafuta, Bwawa la Kuzalisha umeme la Mwalimu Nyerere na mingineyo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here