TAWA na miaka mitatu ya utendaji kazi wenye ufanisi na tija

0
Kamishina wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Kamishina wa uhifadhi, Mabula Misungwi Nyanda.

MAMLAKA ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (Tanzania Wildlife Management Authority – TAWA) katika kipindi cha miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Dkt. Samia Samia Suluhu Hassan, TAWA imeendelea kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia Malengo Makuu matatu yaliyoainishwa katika Mpango Mkakati wa Mamlaka 2021/22 – 2025/26.

Malengo hayo ni Uimarishaji wa Ulinzi wa rasilimali za wanyamapori na malikale Uboreshaji wa Huduma za Utalii pamoja, na Utendaji kazi wenye ufanisi na tija ambapo malengo hayo yalitekelezwa na TAWA imepata mafanikio makubwa ikiwemo kupungua kwa Ujangili wa tembo.

Kwasasa, idadi ya tembo wanaokufa imepungua kutoka mizoga 6 mwaka 2021/22 hadi mizoga watatu (3) Februari 2024. “Mafanikio haya yanatokana kuimarika kwa ulinzi kulikochangiwa na kuongezeka kwa vitendea kazi, morali ya watumishi, mtandao kwa kiitelijensia,”

“Doria za mwitikio wa haraka matumizi ya teknolojia na kufunga visikuma mawimbi ili kufuatilia mienendo ya wanyamapori katika kuhakikisha wanyama wanakuwa salama,” anasema Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) Mabula Misungwi Nyanda.

Kamishna Misungwi anasema, TAWA imeendelea kushirikiana na wananchi katika kutatua migogoro kwenye maeneo ya hifadhi kwa kutekeleza maelekezo ya Serikali yaliyotolewa kupitia Kamati ya Mawaziri nane (8) wa Wizara za Kisekta.

“Kwa kushirikiana na wananchi migogoro mipaka katika Mapori ya Akiba saba (7) ya Swagaswaga, Mkungunero, Wamimbiki, Igombe, Liparamba, Mpanga Kipengere na Selous kati ya nane (8) yaliyotolewa Maelekezo na Kamati ya Mawaziri nane wa kisekta imemalizika ambapo jumla ya vigingi 1,681 vimesimikwa kuzunguka mipaka ya hifadhi,” anasema.

Aidha, katika utatuzi wa migogoro hiyo eneo lenye ekari 103,544.48 limemegwa kutoka kwenye hifadhi na kuwapatia wananchi kwa ajili ya shughuli za kiuchumi. Sambamba na hilo, Serikali kupitia TAWA inaendelea kukamilisha zoezi la kulipa fidia kaya 145 zilizo katika Pori la Akiba Mkungunero.

Nyanda anasema, kutokana na ongezeko la matukio ya wanyamapori wakali na waharibifu kati ya mwaka 2021-2024 TAWA imefanya jumla ya doria siku watu 58,818 kukabiliana na matukio 8,001 yaliyotokea katika Wilaya 73 nchini.

Jitihada nyingine zilizofanyika ili kupunguza madhara kwa maisha ya watu na mali zao ni pamoja na kujenga vituo vituo 16 vya askari katika Wilaya 16 ili kuitikia kwa haraka matukio ya wanyamapori wakali na waharibifu, ununuzi wa pikipiki 50, kutoa mafunzo na kushirikisha askari wa wanyamapori wa vijiji; Village Game Scout na jeshi la akiba wapatao 184.

“Askari waliopata mafunzo ya kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu wanafanya kazi kwenye maeneo sugu ya matukio (Bunda, Busega, Meatu, Same, Lindi, Korogwe, Itilima, Liwale, Nachingwea, Mwanga, na Tunduru);
Kuongeza vituo vya muda vya askari (ranger stations) kutoka 46 hadi 55;Kuongeza idadi ya askari wa kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu kutoka 139 hadi 237” anasema.

Kamishna Misungwi aliongeza, wamejenga mabwawa 10 katika mapori ya akiba Kizigo – 09 (lililopo Manyoni) na Mkungunero – 01 (katika Wilaya ya Kondoa);Wametoa elimu ya uhifadhi na mbinu rafiki za kujikinga na madhara ya wanyamapori wakali na waharibifu kwa wananchi 764,438 katika vijiji 1,319 nchini.

“Tumeimarisha vikundi 179 vya wananchi vya kufukuza tembo na kutoa vifaa vya kufukuza tembo ikiwemo Roman candles 1,320, thunder flashes 1,310, vuvuzela 548, filimbi 288, tochi 524, mbegu za pilipili, mabomu ya pilipili. Tumefunga visukuma mawimbi kwa viongozi wa makundi ya tembo 8 katika Wilaya za Same, Tunduru, Liwale na Nachingwe na kuimarisha mawasiliano kwa kutoa namba ya kupiga simu bure ili kuwezesha wananchi kutoa taarifa mapema.” anasema.

Kutokana na jitihada hizo, anasema madhara hasi ikiwemo idadi ya vifo imepungua kutoka vifo 318 kati ya mwaka 2017-2020 hasi vifo 259 kati ya mwaka 2021-2024 licha ya kuongezeka kwa matukio.

Vile vile, wamefanikiwa kuongeza ushirikishwaji jamii katika shughuli za uhifadhi na kuwezesha miradi ya maendeleo kwa Jamii “TAWA imeendelea kushirikiana na jamii katika shughuli za uhifadhi kwa kuchangia miradi ya maendeleo inayoibuliwa na jamii kwenye maeneo mbalimbali hususan yanayozunguka Mapori ya Akiba.”

“Kati ya mwaka 2021 na 2024 TAWA imechangia miradi ya jamii yenye thamani ya Shilingi Milioni 193.3 ikiwemo; Ujenzi wa Soko la samaki katika mji mdogo wa Ifakara – Kilombero (TSh. Milioni 66) ujenzi wa darasa, ofisi ya walimu pamoja na ununuzi wa madawati katika shule ya Msingi Usinge Kaliua – Tabora (TZS Milioni 50)”

Miradi mingine ni kuchangia madawati 100 katika Wilaya ya Bunda,Ununuzi wa mashine mbili (2) za Kusaga katika Mkoa wa Mara, ukchangia Shilingi Milioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa zahanati na darasa – Mwibara,
Kuchangia Shilingi Milioni 20 kwa ajili ya ujenzi wa Zahanati ya Bungo – Korogwe na kuwezesha jamii kunufaika na Uvuvi na ufugaji nyuki katika Hifadhi.

“TAWA imeweka utaratibu wa kuwezesha jamii kunufaika na shughuli za uvuvi na ufugaji nyuki katika maeneo ya Mapori ya Akiba na Tengefu. Pamoja na kuimarika kwa mahusiano ajira kwa takribani wavuvi 7,511 na warina asali 2,046 jumla ya Shilingi Bilioni 3.98 kutokana na shughuli za uvuvi na ufugaji nyuki katika Mapori ya Akiba ya Rukwa, Ugalla, Uwanda, Moyowosi Kilombero na Inyonga,” anasema Kamishna Nyanda.

Anaendelea kusema, wananchi wamekuwa wakinufaika kwa kuvua wastani wa tani 15 za samaki kwa siku katika pori la akiba Uwanda pekee. Vilevile, kupitia uvuvi Halmashauri ya Sumbawanga imekusanya Shilingi Milioni 303 kupitia leseni na ushuru kutokana na uvuvi kwenye hifadhi katika katika kipindi cha Julai – Desemba 2023.

Anasema, kutokana na shughuli za utalii (utalii wa picha na uwindaji) TAWA imekuwa ikitoa gawio kwa Halmashauri za Wilaya 32 na Vijiji 187. Katika kipindi cha mwaka 2021/22 – 2023/24 jumla ya Shilingi Bilioni 8.95 zilitolewa kwa wanufaika. Pamoja na kuimarisha mahusiano na dhana nzima ya uhifadhi kwa wananchi wanaozunguka maeneo ya hifadhi, fedha hizo zinatumika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo inayoibuliwa na wananchi.

“Mamlaka imekuwa ikisimamia na kurejesha stahili zinazotokana na shughuli za utalii katika maeneo ya Jumuiya za Uhifadhi za Wanyamapori. Kati ya mwaka 2021-2024 jumla ya Shilingi Bilioni 11.91 zilirejeshwa kwa Jumuiya ya Hifadhi za Wanyamapori 13 kwa ajili ya kuendeleza uhifadhi na miradi ya maendeleo kwa vijiji vilivyotoa ardhi yao kuwa hifadhi za wanyamapori.” anasema.

Aidha, Kamishna huyo anasema, kufuatia juhudi za Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutangaza utalii kupitia Filamu ya ‘the Royal Tour,’ kutoa fedha za kuendeleza miundombinu ya utalii na fursa za kutangaza katika masoko ya Kitaifa na Kimataifa mafanikio lukuki yamepatikana.

Miongoni mwa mafanikio hayo ni kuongezeka kwa idadi ya watalii wa picha na uwindaji, ambapo idadi ya watalii wa picha waliotembelea vivutio kutoka 37,684 mwaka 2020/21 hadi 166,964 mwaka 2022/23 na watalii 116,529 hadi Februari 2024.

Wawindaji kutoka 355 mwaka 2020/21 hadi wawindaji 787 mwaka 2022/23 na wawindaji 481 hadi Februari mwaka 2024. Kuongezeka kwa idadi za meli za Kimataifa za utalii kutembelea eneo la Kihistoria Kilwa kutoka meli 4 zilizokuwa na watalii 400 mwaka 2020/21 hadi meli 8 zenye watalii 925.Kuuza vitalu kwa Mnada wa Kieletroniki na kuanza utekelezaji wa Uwekezaji Mahiri.

“Miongoni mwa matunda ya Filamu ya ‘Royal Tour’ ni mwitikio wa mkubwa wa wawekezaji katika mnada wa vitalu vya utalii ambapo jumla ya vitalu 66 vimeuzwa na mapato ya jumla ya Dola za Kimarekani 8,277,000 zilikusanywa ikilinganishwa na Dola 2,405,000 endapo vitalu hivyo vingeuzwa kwa njia ya utawala ikiwa ni ongezeko la Dola 5,872,000,” anasema.

Akifafanua zaidi anasema, Serikali ilikamilisha taratibu za uwekezaji kwa ajili ya kusaini mikataba ya uwekezaji mahiri katika Vitalu vya Ikorongo, Grumeti, Maswa Mbono, Maswa Kimani, Maswa North, Mkungunero na Selous LL1. Mikataba saba ilisainiwa Januari 2024 ambapo kupitia mikataba hiyo Serikali itapata Dola za Marekani Milioni 312. 25 kwa kipindi cha miaka 20 sawa na wastai wa Dola za Marekani Milioni 15.5.

Anasema, kufuatia juhudi hizo idadi ya vitalu uwindaji vyenye wawekezaji imeongezeka kutoka kutoka 59 hadi 68. Kusainiwa na kuanza utelelezaji wa Mikataba ya uwekezaji mahiri – SWICA ambapo jumla ya USD 2,773, 000 sawa na Shilingi Bilioni 7.01 zimekusanywa tangu kusainiwa kwa mikataba ya SWICA Januari 3 mwaka 2024.

Afisa Mwandamizi wa Habari na Mawasiliano kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina, Sabato Kosuri, akizungumza wakati wa Kikao kazi baina ya TAWA na Wahariri.

“Kuimarika kwa ukusanyaji wa maduhuli ya jumla kupitia vyanzo mbalimbali na kuchangia katika Mfuko Mkuu wa Serikali takribani ambapo Jumla ya kiasi cha Shilingi Bilioni 184.74 zimekusanywa kati ya mwaka 2020/21 hadi 2024 Machi 8.

Anasema, kwa kutumia fedha zilizotolewa kwa Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO 19 (Tanzania Social Economic Response and Recovery Plan (TCRP). Miundombinu wezeshi ya Utalii katika maeneo yanayosimamiwa na Mamlaka imeboreshwa ambapo miradi kadhaa imetekelezwa.

Anasema, pamoja na kuboresha miundombinu ya uhifadhi na utalii, TAWA ilijielekeza pia kuweka mazingira wezeshi kwa ajili ya kuongeza ufanisi utendaji kazi. Kupitia bajeti ya Mamlaka ya Maendeleo na fedha zilizotolewa kwa Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO 19 (Tanzania Social Economic Response and Recovery Plan (TCRP).

“Mamlaka imejiimarisha katika matumizi ya mifumo ya TEHAMA katika ukusanyaji wa mapato kupitia mfumo wa MNRT Portal, uandaaji wa bajeti (PlanRep), Matumizi (MUSE), kushughulikia majadala e-office, huduma kwa wateja (chatroom) na mfumo wa kukusanya taarifa za uhifadhi (Conservation Information System), mfumo wa kukusanya taarifa za doeria (Special Monitoring AR Tool)” anasema.

Kamishna huyo anasema, pamoja na mafanikio hayo zipo changamoto kadhaa zinazowakabili ambazo wanaziwekea mikakati mbalimbali ya kuzitatua ikiwemo ongezeko la matukio ya wanyamapori wakali na waharibifu, uvamizi wa maeneo yaliyohifadhiwa kwa shughuli za kilimo na mifugo, kampeni za kupinga uwindaji wa kitalii zinazoongozwa na asasi za kiraia hususan katika nchi ambazo ni masoko makubwa ya uwindaji.

“TAWA itaendelea kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia sheria, kanuni, miongozo na maelekezo ya viongozi mbalimbali wa Wizara na Kitaifa. Kuongeza ubunifu na mbinu mbalimbali kukabiliana na matukio ya wanyamapori wakali na waharibifu,”

“Ulinzi wa rasilimali za wanyamapori na kuongeza mapato pamoja na kushirikiana na wadau na kushiriki katika majukwaa ya Kimataifa kuelezea faida za uwindaji wa kitalii ili kukabiliana na kampeniza kupinga uwindaji. Kutekeleza azma hii muhimu kwa Serikali,

Mamlaka inaongeza nguvu katika matumizi ya teknolojia katika ulinzi na usimamizi wa mapato,” anamaliza Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) Mabula Nyanda, mbele ya wahariri na waandishi wa vyombo vya habari, kwenye mkutano ulioratibiwa na Ofisi ya Msajili Hazina.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here