TANZANIA inashiriki katika msafara wa kunadi vivutio vya utalii katika nchi za Ulaya Magharibi ulioanza Machi 10-15, 2025 ambapo wauzaji na wanunuzi katika sekta ya utalii wanakutana katika msafara huo wenye mawakala zaidi ya 50.
Msafara huo unaojulikana kwa jina la “My Tanzania Roadshow 2025 ” na kuratibiwa na kampuni ya Kili Fair unafanyika katika miji mitano ya Cologne Ujerumani, Antwerp Ubelgiji, Amsterdam Uholanzi, London na Manchester iliyopo nchini Uingereza kunadi vivutio vya Utalii vilivyopo Tanzania ambapo nchi za ulaya ni soko kubwa linaloleta Watalii wengi Tanzania
Akizungumzia Msafara huo Mkurugenzi wa Masoko kutoka Bodi ya Utalii Tanzania Ernest Mwamaja amesema kuwa Wadau na wauzaji wa Mazao ya utalii ukihusisha vyama vya waendesha utalii, wamiliki wa hoteli, makampuni ya ndege kutoka Tanzania wanakutana na wanunuzi wa Utalii (Buyers) kwa ajili ya kufanya biashara.
Mwamaja ameeleza kuwa nchi ya Ujerumani pekee takribani watalii 100,000 wanatembelea vivutio vya Utalii vilivyopo Tanzanka kila mwaka ambapo kupitia misafara ya utalii muitikio wa wadau kushiriki umeendelea kuongezeka kila mwaka.
“Kupitia Misafara hii hasa katika soko la Ulaya magharibi tutaendelea kuwashawishi wageni kuja Tanzania kwa wingi ili tuongeze pato la Serikali, na tunaamini jitihada za kuboresha miundombinu ya utalii zinazoendelezwa na Serikali ya awamu ya sita zitachangia wageni wanaokuja nchini kwetu kukaa siku nyingi zaidi kwa kuwa tuna mtawanyiko wa vivutio vya Utalii katika maeneo mengi” ameeleza Mwamaja.
Katika Msafara huo unaoshirikisha kampuni za Sekta binafsi zaidi ya 50 unajumuisha pia taasisi za Serikali ambazo ni Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Mamlaka ya hifadhi ya eneo la Ngorongoro (NCAA) na shirika za Hifadhi za Taifa (TANAPA) ambazo ushiriki wao unatoa hakikisho kwa sekta binafsi kuwa Serikali inawaunga mkono jitihada zao kwa kuweka mazingira rafiki, kuboresha miundombinu na huduma za utalii kwa wageni wanaotembelea Tanzania.