KATIBU Mkuu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mohammed Khamis Abdulla, amesema kuwa Tanzania imepokea pongezi kutoka kwa mataifa mbalimbali ya Afrika kutokana na mafanikio yake katika kupeleka huduma za mawasiliano hadi maeneo ya vijijini.
Hatua hiyo imeiweka Tanzania kuwa mfano bora wa kuigwa barani Afrika katika uendelezaji wa huduma za kidijitali kwa wote.
Akizungumza wakati wa kufunga Mkutano wa 14 wa Jukwaa la Afrika la Utawala wa Mtandao (AfIGF 2025) uliofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), Abdulla alisema mkutano huo ulijumuisha washiriki kutoka karibu nchi 40 za Afrika waliokusanyika kujadili maendeleo ya teknolojia ya kidijitali na namna ya kufanikisha ushirikishwaji wa kila raia katika zama za kidijitali.
Abdulla alisisitiza kuwa, Tanzania iko tayari kushirikiana na Mataifa mengine kwa kuwapatia uzoefu na mbinu bora za kupeleka huduma za mawasiliano kwa wananchi, hasa waishio vijijini.
Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF). Mhandisi Peter Mwasalyanda alihudhuria mkutano huo na kushiriki mijadala mbalimbali iliyolenga kuanisha mafanikio, changamoto, na fursa zinazohusiana na upatikanaji wa huduma za mawasiliano katika maeneo ya pembezoni.
Ushiriki huo ni sehemu ya juhudi za Serikali kuendeleza majadiliano ya kitaifa na kimataifa kuhusu usawa wa kidijitali.
Kupitia UCSAF, Serikali ya Tanzania imefanikiwa kupeleka huduma za simu na intaneti katika maeneo ya vijiji, maeneo ambayo awali hayakuwa na huduma hizo.
Mafanikio hayo yamekuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika maeneo ya vijijini.